Na mwandishi wetu
Kocha wa zamani wa Yanga SC, Hans Pluijm ameitahadharisha timu hiyo kutowadharau Madeama watakaokutana nao Ijumaa hii kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pluijm ambaye kwa sasa yuko nyumbani kwake Ghana kunakopigwa mechi hiyo, alisema mchezo huo hautokuwa rahisi kwani wanakutana na timu imara yenye wachezaji wenye ari ya kupambana muda wote wa mchezo, hivyo wanapaswa kupambana ili kushinda.
“Ni mchezo mgumu kwa timu zote mbili hasa Yanga ambao lazima washinde kama wanataka kwenda hatua inayofuata ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika,” alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema ameshuhudia mechi mbili za hatua hiyo walizocheza Yanga, walicheza vizuri na kuongoza katika maeneo mengi licha ya kutopata ushindi wakiwa na makosa madogo ambapo anaamini kocha wao, Miguel Gamondi atakuwa ameyabaini na kuyafanyia kazi.
Alisema miamba hiyo ya Tanzania kwa sasa imekamilika kwa kila kitu katika benchi lake la ufundi akiwemo mchambuzi wa picha za video za wapinzani na taarifa zote kuhusu wapinzani wao Medeama, hivyo anaamini wanayo nafasi ya kushinda mechi hiyo.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema kitendo cha Yanga kwenda mapema Ghana kitawasaidia kuzoea hali ya hewa ya joto na unyevunyevu ambayo inahitaji wachezaji waizoee ili kumudu mapambano ndani ya dakika 90 za mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Baba Yara, Kumasi.
Hiyo ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye michuano ya Caf, mara ya kwanza ilikuwa 2016 katika Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi ya kwanza iliyofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam iliisha kwa sare ya bao 1-1 na mchezo wa marudiano Yanga ikafungwa mabao 3-1.