London, England
Kipa wa zamani wa Man United, David de Gea yuko tayari kujiunga na klabu ya Newcastle ambayo ina mpango wa kusajili kipa mwingine baada ya kuumia kwa Nick Pope.
Pope, 31 ambaye pia ni kipa wa timu ya taifa ya England kuumia kwake kumeifanya Newcastle kuingia sokoni na mtu sahihi anayeonekana kuchukua nafasi hiyo ni De Gea ambaye kwa sasa ni mchezaji huru.
De Gea, 33, mwishoni mwa msimu uliopita aliamua kutosaini mkataba mpya Man United hali ambayo iliacha maswali kuhusu wapi anaelekea lakini hadi sasa hajajiunga na timu yoyote.
Awali Newcastle pia ilihusishwa na mipango ya kumsajili kipa mwingine wa England, Aaron Ramsdale anayeidakia Arsenal lakini wamesita kutoa Pauni 50 milioni ambazo Arsenal wanadaiwa kuzitaka.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta pia ametangaza hivi karibuni kuwa hayuko tayari kumuacha Ramsdale aondoke katika timu yake licha ya kuwa kipa huyo aliyetamba msimu uliopita, tangu Septemba hadi sasa amedaka mechi tatu tu akiwa amepoteza nafasi ya kikosi cha kwanza kwa David Raya.
“Nataka Aaron aendelee kuwa nasi, nina furaha ya kuwa na makipa wawili walio bora na Aaron ataendelea kuwa nasi, tunataka kuwa bora, hivyo tunataka kuongeza kwa kile ambacho tayari tunacho, hiyo ndiyo dhamira yetu,” alisema Arteta.