Na mwandishi wetu
Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars inatarajia kushuka uwanjani leo Alhamisi kucheza na Togo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuwania kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon 2024) zitakazofanyika nchini Morocco.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Jumatano kuhusu mchezo huo, kocha mkuu wa Twiga, Bakari Shime (pichani) alisema ameandaa kikosi chake vizuri na kiko tayari kwa mapambano.
“Tunahitaji kushinda kwenda Wafcon kule Morocco, tunatamani kuona uwanja wa nyumbani unakuwa nyumbani. Watanzania wajitokeze kutoa sapoti,” alisema.
Nahodha wa kikosi hicho, Opa Clement amewaahidi Watanzania kuwa watapambana kufa au kupona ili kufanya vizuri.
“Nia yetu ni kufuzu na walimu wamekuwa wakiongea na sisi, kila mchezaji anatamani kucheza na kupata nafasi hiyo ya kuwakilisha taifa,” alisema.
Twiga Stars iliingia raundi ya pili na ya mwisho baada ya kuiondosha Ivory Coast kwa penalti 4-2 baada ya matokeo ya jumla ya sare 2-2.
Togo yenyewe imetoka kushinda jumla ya mabao 13-0 dhidi ya Djibouti. Mchezo wa kwanza walishinda 7-0 na wa pili 6-0. Mchezo wa marudiano baina ya Twiga na Togo utachezwa ugenini Desemba 5, mwaka huu.
Soka Twiga Stars dimbani leo
Twiga Stars dimbani leo
Read also