Na mwandishi wetu
Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema ujio wa kocha Abdelhak Benchikha umerudisha ari ya upambanaji kwa wachezaji na anaamini watafanya vizuri kwenye michuano wanayoshiriki.
Zimbwe alisema kikao cha wachezaji na kocha huyo kilichofanyika kwa mara ya kwanza juzi kimeleta morali mpya na kila mchezaji amekuwa na hamu ya kutaka kuipigania timu kupata mafanikio makubwa.
“Unajua maneno yalikuwa mengi mtaani baada ya kufungwa na Yanga, ndio maana unaona mechi zilizofuata pia dhidi ya Namungo na Asec Mimosas hatukufanya vizuri, kocha Benchikha ametupa moyo na kurudisha ari ya kila mchezaji aliyekata tamaa na ninaamini kiwango chetu katika mechi zijazo kitakuwa cha juu sana,” alisema Zimbwe.
Alisema kwa sasa kambi yao imekuwa na amani, kila mchezaji anafurahia ujio wa kocha huyo na wao kama wachezaji wamekubaliana kumpa ushirikiano wa kutosha ili kubeba mataji na kutimiza malengo ya klabu hiyo.
Simba haijashinda mchezo wowote wa mashindano iliyocheza Novemba, ilicheza mechi tatu, mbili za Ligi Kuu NBC ambapo ilifungwa na Yanga mabao 5-1 na sare ya 1-1 dhidi ya Namungo huku pia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikipata sare dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Soka Benchikha arejesha ari Simba-Zimbwe Jr
Benchikha arejesha ari Simba-Zimbwe Jr
Read also