Buenos Aires, Argentina
Kocha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amemtaka nahodha na mshambuliaji wa timu hiyo, Lionel Messi kuendelea kucheza soka kadri inavyowezekana na kuachana na mpango wa kustaafu.
Messi, 36 kwa sasa anacheza soka nchini Marekani katika Ligi ya MLS na timu ya Inter Miami FC huu ukiwa ndio msimu wake wa kwanza, bado hajasema lolote kuhusu lini hasa atastaafu hasa timu ya taifa.
“Tunamwambia Messi aendelee kucheza kadri atakavyoweza, amedhihirisha bado hajafikia mwisho, hujui ni lini ataachana na soka, ni jambo la kipekee,” alisema.
“Ni mtu mwenye furaha akiwa kwenye uwanja wa soka, na katika hilo nadhani ni vigumu kuwa kama Leo (Messi), uwanjani kwenye mpira ni mahali ambapo anakuwa mwenye furaha,” alisema Scaloni.

Mwaka jana Messi na Scaloni waliiongoza vyema Argentina na kushinda Kombe la Dunia katika fainali zilizofanyika Qatar na baada ya mafanikio hayo kulikuwa na fununu kwamba Messi angestaafu timu ya taifa jambo ambalo hadi sasa hajalifanya.
Messi kwa sasa ni majeruhi baada ya kuumia hivi karibuni wakati akiiwakilisha Argentina katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Brazil, mechi ambayo Argentina ilishinda kwa bao 1-0.
“Sijui kama nimebakisha mengi au machache katika soka lakini kwa mafanikio niliyoyapata kitu pekee nilichobakiza ni kuendelea kufurahia soka, na kwa kuwa niko fiti nitaendelea kushindana katika soka na natumaini itakuwa hivyo kwa muda mrefu,” alisema Messi.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2022, Messi aliibuka mchezaji bora wa fainali hizo na mwezi uliopita alitwaa tuzo ya Ballon d’Or akiwabwaga washindani wake wa karibu, Kylian Mbappe wa PSG na Erling Haaland wa Man City.