Na mwandishi wetu
Makocha wazawa wameeleza maoni yao juu ya ujio wa kocha mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha wakiushauri uongozi wa timu hiyo kumpa muda kuibadili timu ili kufikia mafanikio wanayoyatamani.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema pamoja na wasifu mkubwa wa kocha huyo raia wa Algeria lakini anapaswa kupewa nyezo zote muhimu za kurahisisha kazi ikiwemo wachezaji bora zaidi.
“Huyu ni kocha mkubwa, mzuri tu na ameonesha huko alikotoka, hivyo mwendelezo wake wa yale wanayoyahitaji yanategemea vitu vingi ikiwemo wachezaji wazuri wanaomuelewa, miundombinu bora na kumpa muda afanye kazi yake kwanza,” alisema Mkwasa.
Kocha wa zamani wa Lipuli, Mbao FC, Biashara United, Amri Said ‘Stam’ alisema: “Binafsi kwa miaka mitano iliyopita ndio sasa naona Simba wameleta kocha kweli, kocha huyu ana wasifu na ujuzi wa muda mrefu na kazi yake inaonekana.
“Kidogo tu naona kama mkataba wa miaka miwili waliompa ni mdogo, wangempa angalau kuanzia mitatu maana ni kazi kubwa kuijenga Simba ikae kama ambavyo tunataka, kwa muda uliobaki si rahisi kwake kuleta kombe kubwa ndio maana nasema wangempa muda mrefu atengeneze anachotaka.”
Maoni ya makocha hao hayakuwa mbali na ya kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Mrage Kabange ambaye alikiri uwezo wa Benchikha ni mkubwa, anaonekana ana misimamo na anapenda kuwa na timu bora, hivyo wamwache afanye kazi yake kwa uhuru na upana mkubwa.
“Nimemsikia akizungumza kuwa hataangalia majina ya wachezaji bali atatazama kujituma kwao, anaonekana ana misimamo na anapenda mafanikio kokote anakoenda, sasa ni vizuri uongozi ukamuacha awe huru na apate muda wa kutosha kuirejesha na kuipeleka Simba mbali zaidi,” alisema Kabange.
Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Geita Gold na Tanzania Prisons, Fred Minziro naye alisema anamwona Benchikha ni mpambanaji na ana maono makubwa ya soka, hivyo aachiwe muda aijenge timu kwa ajili ya faida ya mashabiki, wanachama, viongozi na wawekezaji wa timu kwa ujumla.