Na mwandishi wetu
Kocha wa Yanga Miguel Gamondi amesema kuwa amewaandaa vya kutosha vijana wake kwa mbinu mbadala zitakazowaweka salama ikiwezekana kupata ushindi katika mchezo wao na CR Belouizdad ya Algeria.
Yanga kesho Ijumaa itakuwa ugenini Algeria ikitupa karata yake ya kwanza kwenye mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad itakayoanza saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Caf, huku kila upande ukiwa na matumaini ya kushinda mchezo huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya pamoja na ubora wa vikosi vyao.
“Tupo tayari ingawa baadhi ya wachezaji wangu wamefika hapa kwa kuchelewa na uchovu kutokana na majukumu ya timu zao za taifa kuwania kufuzu Kombe la Dunia lakini tutapambana kutafuta ushindi huku tukicheza kwa tahadhari zaidi sababu Belouizdad ni timu nzuri yenye wachezaji bora,” alisema Gamondi raia wa Argentina.
Yanga ambayo msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika inaingia kwenye mchezo huo ikiwa inaonekana kuimarika zaidi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita jambo ambalo limeonesha kuwapa hofu wenyeji wao, Belouizdad ambao hivi karibuni walimfuta kazi kocha wao, Sven Vandenbroeck.
Miamba hiyo inaingia kwenye mchezo huo wakiwa vinara kwenye Ligi Kuu NBC wakikusanya pointi 24 katika michezo tisa lakini ari kubwa waliyonayo ni kushinda mechi mbili zilizopita za ligi ikiwemo ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya watani zao Simba.
Mpaka sasa safu ya ushambuliaji ya Yanga imefunga mabao 26 na kuruhusu mabao matano katika michezo tisa huku wachezaji wake Stephen Aziz Ki na Max Nzengeli wakiongoza kwa kila mmoja akifunga mabao saba.
Belouizdad ambao kikosi chao kinanolewa na kocha Mbrazili, Marcos Paquetá hawana mwenendo mzuri sana kwenye Ligi Kuu Algeria, wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 12 huku wakishinda michezo minne kati ya sita waliyocheza na kupoteza mechi mbili.
Mapungufu makubwa yaliyopo kwenye kikosi cha Bolouizdad ni safu yake ya ulinzi kupitika kirahisi na kuruhusu mabao kwani takwimu zinaonesha katika mechi sita za ligi timu hiyo imefunga mabao tisa na kuruhusu mabao matano.
Katika safu ya ushambuliaji Belouizdad inawategemea zaidi washambuliaji Lamin Jallow raia wa Mali na Merouane Zerrouki wa Algeria ambao wamekuwa na ushirikiano mzuri na uwezo mkubwa wa kufunga mabao.