Na mwandishi wetu
Beki wa zamani wa Man City, Benjamin Mendy ameamua kuifikisha klabu hiyo katika mahakama ya kazi akitaka alipwe mamilioni ya pauni kwa kosa la kumkata mshahara bila ridhaa.
Mendy aliachana na klabu hiyo mara baada ya mkataba wake kumalizika kabla ya msimu huu majira ya kiangazi ikiwa ni baada ya kufikishwa mahakamani kwa makosa ya ubakaji na udhalilishaji kijinsia, makosa ambayo baadaye yalifutwa.
Habari zaidi zinadai kwamba Man City iliacha kumlipa Mendy mshahara wote Septemba 2021 mara baada ya kuhusishwa na tuhuma hizo na kuwekwa rumande.
Taarifa ya jana Jumatatu iliyothibitishwa na wakili mmoja maarufu wa michezo, kesi hiyo ya Mendy ya kutaka alipwe mamilioni ya pauni inatarajiwa kuanza kusikilizwa mapema mwakani.
Baada ya kuachana na Man City, Mendy, 29, alijiunga na klabu ya Lorient inayoshiriki Ligi 1 nchini Ufaransa, huu ukiwa msimu wake wa kwanza na tayari ameshacheza mara tatu zote akitokea benchi.
Kabla ya kujiunga na Man City mwaka 2017, Mendy alikuwa akiichezea Monaco pia ya Ufaransa na akiwa City amebeba mataji ya Ligi Kuu England msimu wa 2018, 2019 na 2021 na mara ya mwisho kuichezea timu hiyo mechi ya ligi ilikuwa Agosti 2021.
Mendy aliwekwa rumande kwa miezi mitano kabla ya kuachiwa kwa dhamana Januari 2022 na kupanda mahakamani mara ya kwanza Agosti 2022 na Januari mwaka huu alifutiwa makosa sita ya kubaka na udhalilishaji kijinsia.
Baadaye mchezaji huyo pia alifutiwa mashtaka ya kumbaka mwanamke mmoja na yale ya jaribio la kumbaka mwanamke mwingine, mashtaka ambayo yote mahakama iliyafuta Julai mwaka huu.
Kimataifa Mendy aipeleka Man City mahakamani
Mendy aipeleka Man City mahakamani
Related posts
Read also