Na Hassan Kingu
Kipigo cha mabao 5-1 ilichokipata Simba mbele ya mahasimu wao Yanga, kimezua taharuki, ni jambo la kawaida hasa inapotokea kipigo kikubwa namna hiyo lakini safari hii aliyejikuta akilaumiwa zaidi ni mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
Wakati Mangungu analaumiwa na kutakiwa aachie ngazi, wapo wanaohoji kulikoni analaumiwa peke yake, vipi kuhusu mwenyekiti wa bodi, Salim Abdallah maarufu Try Again, kwani nini naye halaumiwi na kutakiwa kuachia ngazi.
Na kwa nini lawama anazobebeshwa Mangungu na kutakiwa ajiuzulu hazielekezwi kwa ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Imani Kajula ambaye kimsingi ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za klabu.
Kocha mmoja wa zamani wa Simba alinukuliwa akimtetea Mangungu na kuzungumza kile ambacho pia kimekuwa kikizungumzwa na baadhi ya Wanasimba wanaoona si sahihi kumlaumu Mangungu.
Katika kujenga hoja zao, kocha huyo na kundi linalomtetea Mangungu kwanza wanaona kiongozi huyo kama anatengwa na hivyo wanahoji inakuwaje kiongozi ambaye amekuwa akitengwa hali inapokuwa tete anakuwa wa kwanza kubebeshwa lawama.
Kwa mtazamo wangu si haki kumlaumu Mangungu peke yake mambo yanapoharibika badala yake kila kiongozi anapaswa kubeba mzigo wa lawama lakini pia sishangai wala sioni ajabu kwa wanachama wa Simba kumlaumu Mangungu kwani huo ni utaratibu wa miaka mingi.

Kwa miaka mingi sasa mambo yanapokwenda kombo, mwenyekiti na katibu wake hujikuta katika zigo la lawama na wakati mwingine huwa sababu ya kuondolewa kwenye uongozi hasa inapotokea timu kufungwa mabao mengi.
Na hali inakuwa hivyo kwa kuwa viongozi hao wanachama ndio wanaoshiriki kuwapa ridhaa ya kuongoza klabu kupitia kura, hivyo wana kila sababu ya kumlaumu mtu waliyeshiriki kumuweka katika uongozi.
Kwa hiyo kinachomkuta Mangungu mbali na kwamba ni utaratibu uliozoelekwa kwa miaka mingi lakini pia ni kiongozi ambaye analaumiwa na waliompigia kura badala ya Try Again na Kajula ambao wameingia Simba kwa taratibu nyingine.
Na kimsingi Try Again na Kajula nao wana watu wa kuwalaumu na pengine wameshalaumuwa au hata kuonywa kwa kuzingatia taratibu na makubaliano waliyofikia wakati wanakabidhiwa majukumu ndani ya klabu ya Simba.
Kwa wanachama mtu wanayemjua moja kwa moja ni Mangungu, wao ndio waliomfikisha katika nafasi anayoishikilia na hivyo mambo yanapokwenda kombo wana haki ya kumlaumu na hata kumtaka aachie ngazi na kumpa nafasi hiyo mtu mwingine na wamejiaminisha kwamba huo ndio utaratibu sahihi.

Mabadiko ya mfumo wa kiuendeshaji katika klabu ya Simba bado hayajabadili mtazamo wa wanachama hadi kuamini kwamba Mangungu si kila kitu katika klabu ya Simba bali ni sehemu moja ya uongozi katika klabu hiyo.
Itachukua muda kwa wanachama kuelewa au kukubali ukweli kwamba ndani ya klabu yao kuna watu wengine ambao wana majukumu tena makubwa ya utendaji wa kila siku katika klabu kuliko Mangungu.
Jambo hili likieleweka Mangungu au mwenyekiti yeyote katika Simba atapunguziwa zigo la lawama, ni ama wanachama pia wataanza kumuangalia mtendaji mkuu wa shughuli za klabu, mwenyekiti wa bodi, kocha na wengineo.