Na mwandishi wetu
Bondia Abdallah Pazi au Dulla Mbabe amesema anamsubiri kwa hamu mpinzani wake, Eric Katompa wa DR Congo ili amchape na kulipa kisasi na kuhakikisha bondia huyo harejei tena Tanzania kwa mapambano mengine.
Mbabe (pichani juu) ameyaeleza hayo Ijumaa hii kuelekea pambano la wawili hao litakalopigwa Novemba 25, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.
Pambano hilo ni la pili baina yao ambapo mara ya mwisho mwaka juzi Dulla alikubali kichapo cha pointi kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
“Unajua mimi ni Mzaramo halisi, nina nongwa maana Katompa aliniotea mara ya mwisho na wapo waliouhuzunika na waliofurahi lakini safari hii nimwambie tu namsubiri, nimejipanga vya kutosha.
“Zaidi nafahamu hii ni kama penalti ya mwisho kwangu baada ya kupotezapoteza hivi karibuni, kwa hiyo vyovyote itakavyokuwa nimejipanga, nataka kumtembezea kipigo, nilipize kisasi ili akiondoka nihakikishe harudi tena huku (Tanzania),” alisema Dulla.
Naye muandaaji wa pambano hilo lililobeba maudhui ya ndondi na utalii wa ndani kupitia Kampuni ya Lady In Red, Sophia Mwakagenda alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, akibainisha kuwa Katompa anatarajia kutua Arusha kesho Jumamosi akitokea kwao tayari kwa pambano hilo.