Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya kocha Abdallah Mubiru kutambulishwa timu ya KCCA ya Uganda, kocha huyo amefurahishwa na upambanaji wa wachezaji akiamini ni sehemu nzuri ya kuanzia kupata mafanikio.
Mubiru ambaye msimu uliopita alikuwa akiinoa Mbeya City iliyoshuka daraja, alishuhudia pia mechi ya juzi dhidi ya Vipers na KCCA, mechi ambayo KCCA ilipata ushindi wa 3-1 na kuelezea alichokiona.
“Kwa mfano nimefuatilia hii mechi ya juzi, upambanaji ulikuwa wa kiwango cha juu, kila mtu, kila mchezaji alijitolea kwa uwezo wake kuhakikisha timu inapata matokeo na hiyo inatosha kwangu kwa sababu ninachotaka ni kila mchezaji atoe kilicho bora, na tutaendelea kufanyia kazi hapo kwamba kila mtu ajaribu kuwa bora zaidi ili kupata kilicho bora zaidi katika kila mechi,” alisema Mubiru alipozungumza na mtandao wa timu hiyo.
Mubiru ambaye hii ni mara ya pili anarejea KCCA baada ya kuwepo hapo mwaka 2014, ametua kurithi mikoba ya Mreno, Sergio Traguil aliyepoteza michezo yote minne ya ligi aliyoiongoza timu hiyo.
Kocha huyo aliyewahi pia kuzinoa Police FC, Proline FC na Vipers SC amesaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu hiyo ambayo juzi ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kupoteza mechi tano na kutoa sare moja tangu kuanza kwa msimu huu.
Kwa sasa, KCCA inashika nafasi ya 14 kati ya timu 16 baada ya kukusanya pointi nne ikiwa ni tofauti ya 14 dhidi ya vinara BIDCO Bul FC yenye pointi 18 baada ya kila timu kucheza mechi saba.