Barcelona, Hispania
Baada ya kusota rumande kwa miezi takriban 10, hatimaye beki wa zamani wa Barca na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves anatarajia kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kubaka na udhalilishaji kijinsia zinazomkabili.
Alves, 40, ambaye ameichezea timu ya taifa ya Brazil mara 126, alikamatwa Januari mwaka huu kwa madai ya kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mwanamke mmoja katika klabu ya usiku mjini Barcelona na tangu wakati huo hadi sasa ameendelea kusota rumande baada ya kunyimwa dhamana.
Siku ambayo Alves atapanda kortini bado haijawekwa wazi ingawa mchezaji huyo alikana kufanya kosa lolote na kusisitiza kwamba alikuwa na makubaliano na mwanamke anayedaiwa kumfanyia udhalilishaji huo.
Mahakama ya Barcelona imeona kuna mazingira yanayotosha kumfikisha mahakamani mchezaji huyo wa zamani baada ya maombi ya ofisi ya waendesha mashitaka na wakili wa mwanamke anayedaiwa kufanyiwa udhalilishaji.
Nchini Hispania kesi ya kubaka inachunguzwa kwa kujumuishwa na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia na mtuhumiwa anapokutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kuanzia miaka minne hadi 15.
Alves amezichezea klabu mbalimbali barani Ulaya lakini amepata mafanikio zaidi akiwa Barca kwa kushinda mataj sita ya ligi na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati akikamatwa kwa tuhuma za kubaka, Alves alikuwa akiichezea klabu ya Pumas UNAM ya nchini Mexico ambayo mara tu baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, klabu hiyo ilitangaza kuvunja mkataba na mchezaji huyo.
Kimataifa Alves kortini kujibu tuhuma za kubaka
Alves kortini kujibu tuhuma za kubaka
Read also