Bogota, Colombia
Winga wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz hatimaye ameungana kwa mara ya kwanza na baba yake ambaye alitekwa na kundi la waasi nchini humo.
Shirikisho la Soka Colombia limethibitisha leo Jumanne kuhusu kukutana kwa Luis na baba yake Manuel Diaz ambaye alitekwa na waasi wa kundi la ELN akiwa na mkewe ingawa mkewe alipatikana saa kadhaa baada ya tukio hilo.
Utekaji huo ulifanywa Oktoba 28 na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki katika kituo kimoja cha mafuta kwenye mji wa Barrancas jimbo la La Guajira ambako mzee huyo mwenye umri wa miaka 58 anaishi na mkewe.
Baada ya tukio hilo, Luis aliendelea kuiwakilisha Liverpool na Jumapili alikuwapo katika mechi dhidi ya Brentford kabla ya kurudi Colombia akijiandaa kuiwakilisha timu yake ya taifa ambayo keshokutwa Alhamisi itacheza na Brazil katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Luis katika mechi ya Liverpool alionekana akiwa amevaa fulana yenye maandishi ya kuwasihi waasi wamuachie huru baba yake huku klabu yake nayo ikiwa sambamba naye katika kilio hicho ambacho hatimaye waasi wamekisikia kwa kumuachia huru mzee huyo.
Shirikisho la Soka Colombia lilitoa picha ya baba huyo akiwa na mwanaye katika mitandao ya kijamii, picha hiyo ikiwa na kichwa cha habari kilichosema, ‘we are family’.
Kimataifa Hatimaye Luis Díaz, baba yake wakutana
Hatimaye Luis Díaz, baba yake wakutana
Read also