Na mwandishi wetu
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ameushauri uongozi wa timu hiyo kumuongeza Juma Mgunda kwenye benchi la ufundi wakati huu ambao timu inapitia kipindi kigumu.
Mapema wiki hii uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ baada ya kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao Yanga kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo jana Alhamisi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mkongwe huyo alisema sababu ya kumpendekeza Mgunda ni kutokana na kufahamu vizuri mazingira ya timu na ukaribu aliokuwa nao kwa wachezaji waliopo ndani ya kikosi cha Simba akiamini vinaweza kusaidia kupatikana matokeo mazuri.
“Ushauri wangu kwa viongozi wetu, wamrudishe Mgunda ili akasaidiane na Selemani Matola kipindi hiki ambacho wanatafuta kocha mpya atakayechukua nafasi ya Robertinho, wawili hawa wanaujua ushindani uliopo kwenye ligi lakini pia wanajuana vizuri na asilimia kubwa ya wachezaji, watamsaidia pia hata huyo kocha mpya ajae kumuelekeza baadhi ya vitu,” alisema Kibadeni.
Kibadeni alisema matokeo dhidi ya Yanga, ndiyo yamevuruga akili na ari za wachezaji hivyo ili timu irudi katika hali yake ya kawaida ni lazima apatikane mtu sahihi kama Mgunda azungumze na kuwarudisha mchezoni na timu kupata matokeo mazuri.
Kibadeni alisema maamuzi ya kumtimua Robertinho yalikuwa sahihi, lakini viongozi wanapaswa kutoishia hapo badala yake wanapaswa kupambana haraka iwezekanavyo ili kuleta kocha mkuu atakayeshirikiana na waliopo kurudisha furaha ya Wanasimba.
Tayari uongozi wa juu wa timu hiyo chini ya mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ umesema upo katika hatua za mwisho kumalizana na kocha atakayechukua mikoba ya Robertinho, lengo ni kumpa muda kocha huyo kuiandaa timu kabla ya mchezo wao wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas.