Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Simba, Daniel Cadena amesema haikuwa rahisi kwao kuondoka na pointi moja dhidi ya Namungo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana Alhamisi.
Cadena alisema kuwa pointi moja ilikuwa muhimu zaidi kwao baada ya kutoka kucheza mechi kubwa ambayo walipoteza kwa idadi kubwa ya mabao hivyo ilikuwa ngumu kukaa sawa mapema. Mchezo uliopita Simba ilifungwa mabao 5-1 na Yanga.
“Tulikuwa na nafasi kadhaa za kufunga mabao lakini hatukufanya hivyo, tukamaliza dakika 45 za kwanza tukiwa nyuma na kipindi cha pili tulifanya mabadiliko ya kuwaingiza Moses Phiri, Luis Miquissone na Shaban Chilunda ambao walibadilisha mchezo.
“Nililazimika kuwachezesha washambuliaji wengi baada ya Namungo kucheza zaidi kwenye eneo lao, hivyo sikuhitaji viungo wengi, nilihitaji washambuliaji ili kuongeza presha kwao jambo lililosaidia tukapata bao la kusawazisha,” alisema Cadena.
Kocha wa Namungo Denis Kitambi alisema kupata pointi moja dhidi ya Simba lazima awapongeze wachezaji wake kwa kucheza na mkatati ambao waliingia nao kwenye mchezo huo na walifanikiwa kwa kiasi chake.
“Kwanza kabla ya mchezo nilikuwa naangalia mtindo wa uchezaji wa Simba ambao kipindi cha pili wamefunga mabao tisa na saba kati ya hayo wamefunga katika dakika 30 za mwisho hivyo kwenye dakika 30 za mwisho nilijua tutapata presha sana ndio kitu kilichotokea wamepata bao la kusawazisha.
“Niwe mkweli ungeniuliza siku mbili kabla ya huu mchezo kuwa ningeshukuru sana kuondoka na pointi moja lakini ndani ya dakika 90 kuna nafasi mbili tulitengeneza ambazo kama tungezitumia tungeondoka na ushindi,” alisema Kitambi.