Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema siri ya ushindi wanaoupata kwenye mechi ngumu za Ligi Kuu NBC ni wachezaji wake kucheza kwa kujitoa kuipambania timu yao.
Baada ya kuifunga Simba mabao 5-1, Jumapili iliyopita mabingwa hao watetezi jana Jumatano waliendelea kukusanya pointi tatu baada ya kuifunga Coastal Union bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Akizungumzia mchezo huo, Gamondi alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kucheza kwa kujilinda muda mrefu lakini ari ya upambanaji waliyokuwa nayo wachezaji wake pamoja na mabadiliko aliyoyafanya ndiyo yamesaidia kuchukua pointi tatu nyingine wakiwa ugenini.
“Nina furaha kupata pointi tatu, ukweli mchezo ulikuwa mgumu. Coastal walicheza kwa kujilinda muda wote kitu ambacho kilitusumbua, lengo letu lilikuwa kupata bao la mapema ili kuufungua mchezo lakini haikuwa hivyo ukizingatia wachezaji wangu walikuwa na uchovu mkubwa kutokana na kupumzika siku chache baada ya mechi ya Simba lakini wamekuwa jasiri kwa kucheza kwa kujituma na kupata ushindi,” alisema Gamondi.
Naye Kocha Msaidizi wa Coastal, Fikiri Elias alisema ubora waliokuwa nao wachezaji wa Yanga ndiyo umechangia wao kupoteza mchezo huo ambao kusudio kubwa ilikuwa ni kushinda.
Alisema pamoja na kufungwa lakini wachezaji wake walifuata vyema mbinu ambazo walipanga kuzitumia katika mchezo huo na makosa madogo yaliyotokana na ubora wa wachezaji wa Yanga ndivyo viliwagharimu na kujikuta wanapoteza mchezo huo wakiwa nyumbani.
“Nawapongeza wachezaji wangu walicheza vizuri hasa katika mpango wetu wa kujilinda lakini nawapongeza na Yanga lazima niseme jamaa wana timu bora sana na hilo ndiyo limewapa ushindi lakini naomba mashabiki wetu wasikate tamaa, matumaini yangu timu itafanya vizuri sababu kuna mabadiliko makubwa kadri wanavyocheza,” alisema Elias.