Na Hassan Kingu
Yanga imezidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya ushindi wake mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Simba katika mchezo uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Hakuna aliyeamini kwa kilichotokea, hata Yanga waliopata ushindi hawakuamini kama wangewafunga watani zao katika mechi ngumu kama hiyo kwa idadi kubwa ya mabao mengi kama hiyo.
Mechi iliyokuwa ikimtafuta nani anakwenda kukaa kinara katika msimamo haikutarajiwa kuisha hivyo. Kuichapa Simba ‘unbeaten’ kiasi hicho haikuwa suala rahisi lakini soka huwa lina matokeo yake binafsi yasiyotarajiwa, ukatili usiopimika na mambo mengi ya kustaajabisha.
Manula karudi na mkosi?
Miongoni mwa yaliyostaajabisha ni Simba kuamua kumtumia kipa wao bora kwa sasa, Aishi Manula na kuwaacha makipa wengine watatu benchi ambao miongoni mwao wawili; Ayoub Lakred na Ally Salim wametumika katika mechi za awali msimu huu.
Manula ametoka kwenye majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa kipindi kirefu. Baada ya mechi za kirafiki za mazoezini za wiki chache zilizopita, anarejea kwenye mechi ngumu kama hiyo na anajikuta akiruhusu mabao matano!
Baadhi ya wachambuzi na mashabiki wa soka kiujumla wamekuwa na maswali juu ya hilo lakini mwisho maamuzi ya benchi la ufundi yanaheshimika.
Simba haikuwahi kufungwa mabao zaidi ya mawili tangu kuanza kwa msimu huu lakini kurejea langoni kwa kipa tegemeo Tanzania, Wekundu hao wameruhusu mabao matano.
Doa hili linaweza kuwa gundu kwa Simba katika msimu mzima uliobaki au pengine ikageuka ‘kafara’ ya ushindi na mafanikio yao yajayo ya michuano wanayoshiriki msimu huu.
Hiyo pia ikitegemeana na hasira na maumivu yao yatakayogeuka kuwa usongo wa kufanya vizuri na kurekebisha mambo au kuvunjika moyo kabisa na kuendelea kuzivaa aibu mbele ya safari!
Aziz Ki achanja mbuga
Baada ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki kufunga bao maridadi mbele ya mabeki watatu waliokuwa wakimzongazonga, amefikisha idadi ya mabao saba na kumpiku Jean Baleke wa Simba aliyekuwa amelingana naye.
Kwa kauli nyingine unaweza kusema kiungo huyo hazuiliki msimu huu, amewaka, amezidi kuonesha thamani yake tangu kwenye mechi za mwisho za Yanga msimu uliopita.
Anafunga kila kukicha licha ya nafasi yake kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho huku akiwa tayari ametunukiwa tuzo ya mchezaji bora mwezi Oktoba baada ya kufunga mabao manne katika mechi nne katika mwezi huo.
Kutokana na moto alionao yawezekana yakajirudia ya kiungo huyo kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu NBC msimu huu baada ya kufanya hivyo katika Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu wa 2021-22 alipokuwa akiitumikia Asec Mimosas kabla ya kujiunga na Yanga msimu uliopita.
Maxi, Kibadeni na Diarra
Siku ya mechi hiyo ilibaki kidogo kiungo wa pembeni wa Yanga, Maxi Nzengeli aifikie rekodi adimu ya mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni aliyefunga ‘hat-trick’ pekee tangu mechi za watani zilipoanza kuchezwa.
Ni hivi, wakati Yanga inaongoza mabao manne, Maxi alishafunga mawili na kisha kutokea penalti baada ya beki wa Simba, Henock Inonga kumchezea madhambi Maxi ndani ya 18 kwenye harakati ya kuandika bao la tano.

Mashabiki wa Yanga walitamani Maxi afunge mkwaju huo wa penalti ili mechi iishe na heshima ya mabao mengi na hat-trick moja na pia rekodi ya Kibadeni ifikiwe na mzani uwe sawa baina ya wapinzani hao.
Hata Maxi mwenyewe awali alionekana kutamani kufanya hivyo kabla ya Pacome Zouzoua kuchukua mpira na kuukwamisha wavuni kwa penalti safi na kuendelea kuiweka kileleni rekodi hiyo ya Mzee Kibadeni ya mwaka 1977, Simba iliposhinda mabao 6-0.
Kingine, penalti hiyo endapo ingefungwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra basi Yanga ingekuwa imelipa kisasi kamilifu cha mabao 5-0 cha miaka 11 iliyopita kwani bao moja lilifungwa kwa penalti na kipa wa Simba wakati huo, Juma Kaseja.
Pacome mpya kila mechi
Pacome ni miongoni mwa wachezaji wanaozidi kung’ara kila baada ya dakika 90 za mechi za Yanga na sasa ni kama vile amejihakikishia namba kwenye kikosi hicho cha Miguel Gamondi kutokana uwezo anaoonesha tangu atue msimu huu akitokea Asec Mimosas.
Katika mechi na Simba, ukiachana na kufunga bao la tano lakini bao la pili na la tatu ya timu hiyo, mpira ulianza kupikwa kwake kabla ya kufika kwa anayepiga pasi ya mwisho na kuzaa mabao.
Ujanja, ‘kuendesha timu’ kutoka eneo la katikati, kupiga pasi, chenga na uwepo wake katika matukio muhimu vilitosha kuonesha umma kuwa alistahili kuwa mchezaji bora wa ligi msimu uliopita huko Ivory Coast.
Namba tano ina kitu Kariakoo
Ukiachana na Yanga kulipa kisasi hicho kilichodumu kwa miaka 11, ikumbukwe hata siku ambayo Yanga inachezea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Simba ilikuwa ni Jumapili ya Mei 6, 2012.
Ukiachana na kufanana kwa siku za Jumapili, Yanga ilichezea kipigo hicho mwezi Mei yaani mwezi wa tano na Simba imechezea kipigo kizito Novemba 5. Yaani wakati ule ilikuwa mwezi wa tano na jana ilikuwa tarehe tano!
Wataalam na wenye imani na masuala ya namba wanaweza kuwa na majibu zaidi kuhusiana na hilo lakini wakati mwingine tutaangazia zaidi kitakachotokea ikitokea timu hizi zikakutana Jumapili ambayo ndani yake ina namba tano.
Yanga haijabahatisha
Msimu huu yawezekana Yanga ina kitu inataka kukionesha kwa umma maana ushindi huo wa mabao matano ni ushindi wake wa nne katika mechi 12 za mashindano inayoshiriki msimu huu.
Katika ligi pekee imefanya hivyo mara tatu baada ya kuwa tayari ilishaziadhibu KMC na JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kila mmoja kabla ya kuifanyia unyama huo Simba.
Kwenye soka, ushindi mnono hutokea lakini hauwezi kuwa wa mfululizo mfano Yanga katika mechi nane za ligi tayari imeshinda tatu kwa mabao matano, hivyo kuna ishara ya ushindi huu kwenye mechi lukuki zilizosalia za Wanajangwani hao na kuonesha kuwa hata hizo tatu haikuwa bahati.