Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Jonas Mkude amesema ushindi wa mabao 5-1 walioupata Jumapili dhidi ya Simba umewapa nguvu ya kufanya vizuri na kutetea kwa mara ya tatu taji la Ligi Kuu NBC msimu huu.
Mkude ambaye ametua Yanga msimu huu akitokea Simba, alisema lengo lao kubwa ilikuwa ni kushinda mechi tatu ngumu zilizopita dhidi ya Singida FG, Azam FC na Simba na hilo limefanikiwa hivyo kilicho mbele yao kwa sasa ni kuongeza juhudi na umakini ili kuendelea kupata matokeo mazuri.
“Ni jambo zuri kushinda mechi ya watani lakini kocha amekuwa akitusisitiza kutobweteka baada ya kushinda mechi hizo tatu kwani hazitoshi kutupa ubingwa badala yake tuendelee kupambana katika mechi nyingine ili kuongeza pointi zetu,” alisema Mkude.
Akizungumzia nafasi yake Yanga, alisema pamoja na kukosa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza lakini anafurahi namna kocha anavyogawa muda wa kucheza kwa wachezaji akiamini kadri siku zinavyokwenda atapata nafasi ya kuanza kikosini.
Alisema kocha ndiye mwenye maamuzi ya kuchagua mchezaji wa kucheza na yeye analiheshimu hilo, atakachofanya ni kuendelea kujituma kwenye uwanja wa mazoezi ili kumshawishi kocha aweze kumuamini na kumpa nafasi ya kuanza.
Katika mchezo uliopita dhidi ya Simba, Mkude aliingia dakika saba za mwisho na katika mchezo huo alionesha uwezo mkubwa ikiwemo kuchangia kupatikana kwa bao la tano lililofungwa kwa penalti na Pacome Zouzoua.