Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Hemed Morocco amesema hali ya kukosa ushindi mfululizo katika timu hiyo inatokana na kikosi chake kukosa wachezaji wenye ubora wa kupambana katika Ligi Kuu NBC.
Morocco ameyasema hayo baada ya timu hiyo kukosa ushindi katika mechi zake nane mfululizo kati ya tisa ilizocheza mpaka sasa, hali iliyopelekea Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita, Zahara Michuzi kumtaka kocha huyo kuonana naye kuwaeleza juu ya matokeo hayo mabaya ya timu hiyo.
Akizungumza na GreenSports leo Jumatano, Morocco alisema hajawahi kuwa na matokeo mabovu kiasi hicho lakini ubora mdogo wa wachezaji unachangia matokeo hayo na sasa akijipanga kuongeza idadi ya wachezaji wanne mpaka watano katika usajili wa dirisha dogo ili kuhakikisha wanakuwa bora mzunguko wa pili.
“Hii hali haijawahi kunitokea kabla lakini ni matokeo ya mpira ambayo nafikiri ni kutokana na kukosa wachezaji wenye ubora wa kupambana kwenye ligi ndio maana tuna mpango wa kuongeza wachezaji wanne mpaka watano kwa ajili kuongeza nguvu mzunguko wa pili,” alisema Morocco.
Alisema kwa mechi za kwanza wachezaji hao walionesha ubora mkubwa lakini wamekuwa wakishuka viwango kadri siku zinavyosonga na zaidi makosa ya mchezaji mmoja mmoja ndio yamekuwa yakiwagharimu.
Kocha huyo alipoulizwa kama alishakutana na Mkurugenzi Michuzi alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa ameamua kukaa kimya.
Geita ambayo imeshinda mechi moja, sare nne na kufungwa mara nne, inashika nafasi ya 15 kati ya timu 16 ikiwa na pointi saba.