Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu (pichani) ameipa timu yake asilimia 95 kuibuka na ushindi katika mchezo wa keshokutwa Jumapili wa Ligi Kuu NBC dhidi ya mahasimu wao Yanga.
Miamba hiyo ya soka la Tanzania itakutana kwa mara ya kwanza msimu huu katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku kila upande ukijitapa kuwapa furaha mashabiki wake kwa kuibuka na pointi tatu.
Akizungumza na GreenSports, Mangungu alisema ahadi yake ya kuifunga Yanga mpaka atakapoondoka madarakani inaendelea tena Jumapili na hiyo ni kutokana na maandalizi bora ambayo timu yao imefanya na ari waliyokuwa nayo wachezaji wao.
“Sioni hata sare kwa Yanga, mchezo huu ni muhimu sana kwetu Simba kutokana na maandalizi tuliyofanya lakini kingine sisi ndio wenyeji wa mchezo na tunaingia na rekodi ya kuwa timu pekee ambayo hatujapoteza mchezo tangu msimu uanze, hii inatupa nguvu ya kupambana na kushinda mechi hiyo,” alisema Mangungu.
Alisema kwa upande wao viongozi wameshafanya kazi yao, kilichobaki sasa ni benchi la ufundi na wachezaji kuipambania timu yao ya Simba, kupata pointi tatu na kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo tangu msimu ulipoanza.
Mangungu alisema wanatambua mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani wao lakini yeye na viongozi wenzake wana imani kubwa na kocha wao Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwamba atawapa vijana wake mbinu zitakazowapa ushindi.
Katika kampeni za kuwania kurudi madarakani Mangungu aliwaomba mashabiki wanachama wa timu hiyo kumpigia kura ili awe mwenyekiti wao na yeye atahakikisha anawapa furaha kwa kuifunga Yanga katika kipindi chote cha miaka minne atakachokuwa madarakani.