Barrancas, Colombia
Serikali ya Colombia imesema kuwa Manuel Díaz ambaye ni baba wa mchezaji wa Liverpool, Luis Diaz (pichani) ametekwa na waasi wa Chama cha National Liberation Army (ELN).
Utekwaji wa Manuel Diaz ulifanyika Jumamosi ambapo waasi hao wakiwa na silaha walimteka akiwa na mkewe, Cilenis Marulanda ambaye aliachwa kwenye gari na waasi hao kutokomea na mumewe.
Wanajeshi zaidi ya 120 pamoja na polisi walianzisha msako siku moja baada ya tukio hilo na mamlaka nchini Colombia zimeahidi kutoa Pauni 40,000 kwa mtu atakayewezesha kupatikana kwa baba wa Luis Diaz.
Awali taarifa ya polisi ilihusisha tukio hilo na makundi ya wahalifu lakini jana Alhamisi, serikali ambayo imekuwa katika mazungumzo ya amani na waasi wa ELN, ilidai kuwa ina taarifa za kundi hilo la waasi kuhusika na utekaji huo.
ELN ni kundi la waasi nchini Colombia ambalo limekuwa likijiendesha tangu mwaka 1964 na limekuwa vitani na serikali likidaiwa kuwa na wafuasi wapatao 2,500 na lina nguvu zaidi katika mji wa mpakani na Venezuela.
Manuel Diaz na mkewe walitekwa na watu waliokuwa na silaha katika mji wa La Guajira baada ya kusimama kwenye kituo cha mafuta na kamera za CCTV ziliwaonesha watekaji wakiwa kwenye pikipiki ambao walikuwa wakilifuatilia gari alilokuwa Manuel Diaz na mkewe.
Watekaji hao baadaye walilitelekeza gari likiwa na mama yake Luis Diaz wakati polisi wakiwakaribia lakini walitokomea na Manuel Diaz.
Msako dhidi ya watekaji unaendeshwa zaidi katika maeneo ya mpakani na Venezuela na tayari pikipiki mbili zimekamatwa pamoja na gari moja ambalo polisi wanadhani vilitumika katika utekaji ingawa bado hawajaweza kumpata baba wa Luis Diaz.
Jumanne iliyopita mamia ya watu waliandamana wakiwa na Cilenis Marulanda wakitaka Manuel Diaz aachiwe huru na waasi wakati Liverpool, klabu anayoichezea Luis Diaz ilitangaza kuwa ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Nottingham wanautoa kama heshima kwa Luis Diaz.
Kimataifa ‘Baba wa Luis Diaz ametekwa na waasi’
‘Baba wa Luis Diaz ametekwa na waasi’
Read also