Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imesema kuwa hawana mpango wa kumuachia mshambuliaji wao Moses Phiri kwenye dirisha lijalo la usajili licha ya kuwa hapati muda wa kutosha wa kucheza katika kikosi hicho.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza hayo baada ya tetesi kuwa nyota huyo anahitaji kuondoka katika timu hiyo huku akitajwa kutakiwa na watani wao wa jadi, Yanga SC.
Phiri ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili na Simba tayari ametumikia msimu mmoja huu ukiwa msimu wa pili tangu alipotua nchini akitokea timu ya Zanaco ya Zambia.
“Ni kweli kuna taarifa tunaziona juu ya Phiri, ukweli ni kuwa mchezaji huyo bado ataendelea kubaki ndani ya klabu.
“Suala la kupata nafasi ya kucheza liko chini ya kocha Robertinho (Roberto Oliveira), ukizingatia kuna mechi nyingi na tuna imani Phiri au mchezaji yeyote ndani ya Simba atapata nafasi ya kucheza,” alisema Ally.
Mshambuliaji huyo msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao 10 kwenye Ligi Kuu NBC kabla ya kuanza kusumbuliwa na majeraha ambapo msimu huu hadi sasa amefunga mabao matatu.
Katika hatua nyingine Ally alisema kuwa kikosi chao kimeingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Yanga, utakaochezwa Jumapili ya Novemba 5, mwaka huu.
Alisema mipango yao ni kutafuta pointi 15 za awamu ya pili katika michezo mitano iliyopo mbele yao huku wakianza na pointi tatu dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC.