Riyadh, Saudi Arabia
Saudi Arabia ndio nchini pekee iliyoomba kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2034 na hivyo inapewa nafasi kubwa ya kuandaa fainali hizo baada ya Australia kutangaza kujitoa.
Chama cha Soka Australia kilithibitisha uamuazi wake wa kujitoa katika mbio hizo saa chache kabla ya jana Jumanne ambayo ni siku ya mwisho iliyowekwa na Fifa kwa nchi kuthibitisha nia ya kuandaa fainali hizo.
“Tumefikia hitimisho la kutoomba kuwa wenyeji katika michuano ya 2034,” ilieleza taarifa ya Chama cha Soka Australia.
Badala yake chama hicho kimetangaza nia yake ya kuweka nguvu katika mpango wa kuandaa fainali za Kombe la Asia kwa wanawake mwaka 2026 pamoja na Kombe la Dunia la Klabu kwa mwaka 2029.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinatarajia kufanyika katika nchi za Marekani, Mexico na Canada wakati Moroco, Ureno na Hispania zitakuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2030 ambapo pia mechi nyingine tatu za fainali hizo zitafanyika katika nchi za Argentina, Paragua na Uruguay.
Awali Fifa walidai kuwa fainali za Kombe la Dunia 2034 zingefanyika kati ya Asia au Oceania na nia ya Australia kutaka kuwa mwenyeji ilionekana kama ndio nchi pekee ambayo ingeweza kushindana na Saudi Arabia katika mbio hizokabla ya kutangaza kujitoa katika hatua za mwisho.
Saudi Arabia pamoja na kulalamikiwa kwa kukiuka haki za binadamu lakini inapewa nafasi kubwa ya kuandaa fainali hizo katika ubora hasa baada ya Qatar iliyotiliwa shaka kufanikiwa kuandaa fainali hizo mwaka jana kwa mafanikio makubwa.
Kimataifa Saudi Arabia mwenyeji Kombe la Dunia 2034
Saudi Arabia mwenyeji Kombe la Dunia 2034
Read also