Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya ameeleza kuwa wamejipanga kuondoka na pointi tatu dhidi ya Simba kwani hawako tayari kupoteza mchezo wa tatu mfululizo dhidi yao.
Yanga imepoteza michezo miwili dhidi ya Simba kwenye mashindano tofauti, ikiwemo mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita kwa kichapo cha mabao 2-0 na Ngao ya Jamii iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 3-1.
Mudathir alisema kikosi chao kimeendelea kuimarika na kitendo cha kushinda michezo mitatu iliyopita kwenye ligi baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu kimeongeza morali kikosini mwao kuelekea mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu Afrika.
“Hii ni mechi kubwa, maandalizi yanaendelea vizuri tunahitaji kupata matokeo mazuri ya alama tatu kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo na mwisho wa msimu kutetea taji letu.
“Maandalizi yako vizuri hatutakuwa tayari kuona tunaenda kupoteza huu mchezo kwa mara nyingine, tuko imara na mashabiki wajitokeze kusapoti timu ili kuendeleza ushindani,” alisema Mudathir.
Mechi baina ya wababe hao inatarajiwa kupigwa Novemba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 18, sawa na Simba ambayo imezidiwa idadi ya mabao ya kufunga huku Yanga ikiwa imecheza mechi saba, Simba imeshuka dimbani mara sita mpaka sasa.