Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na Inter Miami FC ya Marekani, Lionel Messi ameibuka kinara wa tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya nane na kumbwaga mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland ambaye pia alikuwa akipewa nafasi ya kubeba tuzo hiyo.
Messi alipewa tuzo hiyo Jumatatu hii usiku katika hafla iliyofanyika jijini Paris, akibebwa na mafanikio ya Argentina aliyoiongoza kubeba Kombe la Dunia mwaka jana katika fainali zilizofanyika Qatar.
Wakati Messi akiibeba tuzo hiyo, kiungo wa England na klabu ya Real Madrid ya Hispania, Jude Bellingham ametwaa tuzo ya mwanasoka bora kijana wa umri chini ya miaka 21 maarufu Kopa Trophy.
Mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe ambaye alifunga hat trick katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina, katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or msimu huu ameshika nafasi ya tatu nyuma ya Haaland.
“Ni jambo zuri kuwa hapa kwa mara nyingine kufurahia tukio hili, kufanikiwa kubeba Kombe la Dunia pamoja na kutimiza ndoto yangu,” alisema Messi, nyota wa zamani wa Barcelona na PSG.
“Sikuweza kufikiria kwa namna nilivyopitia katika maisha yangu ya soka na kufanikiwa kushinda kila kitu nilichoshinda, bahati niliyo nayo ya kuwa katika timu bora ya kihistoria,” alisema Messi.
Kwa upande wa Haaland ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Norway ambaye ana rekodi ya kufunga mabao 36 katika mechi 35 za mashindano yote msimu uliopita na ambaye ameisaidia Man City kubeba mataji matatu ya Ligi Kuu England, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya, amepewa heshima kwa tuzo ya Gerd Mulller kwa kuwa mfungaji bora.
“Napenda kuwashukuru Manchester City, klabu yote, pia napenda kuishukuru familia yangu na watu wote walio karibu nami kwa kuniwezesha kufika hapa nilipo leo,” alisema Haaland.
Messi kwa sasa ndiye anayeongoza kwa kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mara nyingi akiwa amefanya hivyo mara nane na kumzidi mpinzani wake Cristiano Ronaldo ambaye mara ya mwisho alitwaa tuzo hiyo mwaka 2017.
Ronaldo ambaye ametwaa tuzo hiyo mara tano, safari hii jina lake halikuwamo katika orodha ya wachezaji waliotajwa kuwania tuzo hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2003.
Kipa wa Argentina na klabu ya Aston Villa, Emiliano Martinez yeye ametwaa tuzo ya kipa bora maarufu Yashin Trophy
Martinez hata hivyo alijikuta katika wakati mgumu katika hafla ya utoaji tuzo hiyo kwa baadhi ya watu kuguna kwa kinachoaminika kuwa mashabiki walio wengi hawakufurahia aina ya ushangiliaji wake kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Vinicius Jr
Naye mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior yeye alipewa tuzo ya Socrates kwa mchango wake wa nje ya uwanja na kuahidi kuendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi baada ya kujikuta akisakamwa na kadhia ya ubaguzi.
Vinicius Jr amepewa tuzo hiyo kwa kuanzisha taasisi ambayo inajenga shule kwenye maeneo ya watu wanaoishi katika mazingira magumu na pia amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye elimu kwao nchini Brazil.
“Nitaendelea kuwa imara katika kupiga vita ubaguzi wa rangi, inasikitisha kuzungumzia habari za ubaguzi wa rangi siku hizi, lakini tunalazimika kuendelea na vita hii ili watu wasiathiriwe kwa sana,” alisema Vinicius.
Kiungo wa zamani wa Man United, Real Madrid na timu ya taifa ya England, David Beckham ndiye aliyemkabidhi Messi tuzo ya Ballon d’Or lakini kabla ya kumkabidhi alitoa salamu za heshima kwa marehemu Sir Bobby Charlton.
Sir Bobby Charlton ambaye alifariki dunia hivi karibuni akiwa na miaka 86 alikuwamo katika kikosi cha England kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 1966.
Orodha ya wanasoka waliowania Ballon d’Or ni kama ifuatavyo…
Lionel Messi
Erling Haaland
Kylian Mbappe
Kevin De Bruyne
Rodri
Vinicius Jr
Julian Alvarez
Victor Osimhen
Bernardo Silva
Luka Modric
Ballon d’Or Wanawake
Naye kiungo wa timu ya wanawake ya Barcelona, Aitana Bonmatí (pichani chini) ameshinda tuzo ya Ballon d’Or kwa upande wa wanawake akibebwa na mafanikio yake katika timu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Hispania.
Bonmatí, 25 ameiwezesha Barca kubeba taji la Ligi Kuu ya Wanawake Hispania au Liga F pamoja na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya na zaidi ya yote aliisaidia hispania kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC).

Katika fainali za WWC zilizofanyika hivi karibuni katika nchi za Australia na New Zealand aliibuka mchezaji bira na hivi karibuni Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) ulimpa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mwanamke.
Katika tuzo ya Ballon d’Or, Aitana aliwabwaga mshambuliaji wa Australia, Sam Kerr pamoja na winga wa Hispania, Salma Paralluelo.
Hongera sana messi hiyo sio kazi ndogo