Barrancas, Colombia
Wanajeshi zaidi ya 120 nchini Colombia wanaendesha operesheni kumsaka Luis Manuel Diaz ambaye ni baba wa mshambuliaji wa Liverpol, Luis Diaz (pchani) na tayari mamlaka zimetangaza kutoa Pauni 40,000 kwa atakayesaidia kupatikana kwa mzee huyo.
Wanajeshi hao pamoja na polisi wameanza kufanya msako huo Kaskazini mwa Colombia kuanzia jana Jumapili wakimsaka baba wa mchezaji huyo ambaye awali alitekwa yeye na mkewe aitwaye Cilenis Marulanda.
Baadaye Jumapili hiyo hiyo Cilenis ambaye ndiye mama wa Luis Diaz taarifa za kupatikana kwake zilitolewa ikidaiwa kwamba mama huyo alipatikana Jumamosi akiwa Barrancas.
Kutokana na tukio la kutekwa kwa wazazi wake, Luis Diaz, 26, aliikosa mechi ya Jumapili ambayo Liverpool ilicheza na Nottingham Forest na kutoka na ushindi wa mabao 3-0.
Taarifa ya jeshi ilieleza kuwa katika mpango wa kumsaka mzee huyo wameweka vizuizi barabarani huku wakitumia helikopta, ndege pamoja na rada katika zoezi hilo.
Mamlaka za kiserikali nchini Colombia hazijaweka wazi kwa undani kuhusu utekaji huo lakini vyombo vya habari nchini humo vilidai kwamba baba na mama wa Luis Diaz walitekwa wakiwa katika kituo kimoja cha mafuta mjini Barrancas.
Mwanasheria mkuu wa serikali nchini Colombia, Francisco Barbosa aliwasiliana na Luis Diaz mara mbili na kumpa taarifa za uchunguzi wa kutekwa kwa mzazi wake.
Barbosa alimwambia mchezaji huyo kuwa taarifa walizonazo ni kwamba kuna uwezekano baba yake yuko nchini Venezuela na hivyo watahitaji ushirikiano na mamlaka za nchini humo.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema kwamba ushindi wa mabao 3-0 walioupata katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Nottingham Forest unakuwa heshima kwa Diaz.
Klabu ya Liverpool ilieleza kufahamu tukio hilo na katika mechi na Forest, mchezaji wa Liverpool, Diogo Jota akiwa amezungukwa na wachezaji wenzake aliinua juu jezi yenye namba 7 kama kuonesha mshikamano wao kwa Luis Diaz.
Kimataifa Wanajeshi 120 Colombia wamsaka baba wa Luis Diaz
Wanajeshi 120 Colombia wamsaka baba wa Luis Diaz
Read also