Na mwandishi wetu
Kocha wa Namungo, Denis Kitambi amesema siri ya kupata ushindi wa mabao 3-1 jana dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex ni kutengeneza nafasi kwa kushtukiza, mtego ulioshindwa kuteguliwa na wapinzani wao.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Namungo msimu huu baada ya awali kupoteza mechi tatu na sare tatu na sasa ikiwa imekusanya pointi sita na kukwea mpaka nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Kitambi alisema anawapongeza vijana wake kwa kushinda mchezo huo kwani hali yao ilikuwa mbaya na hiyo imetokana na kujituma kwao, akiwasihi waendelee kupambana zaidi kwenye mechi zinazofuata.
“Kikubwa mechi tulivyoiangalia kama benchi la ufundi siyo kuhusu mbinu wala mkakati, tuliwaambia vijana tuko kwenye wakati mgumu, twende tukapambane tukawaonyeshe kuwa bado tuna nia ya kuiweka timu yetu kwenye nafasi nzuri.
“Nashukuru kwa hilo, wachezaji wamejituma sana, yalikuwa ni mabao mazuri ya mipira ya kushtukiza katika hali kama hii tuliyokuwa nayo hali ya kujiamini inapokuwa chini ni lazima ucheze kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza,” alisema Kitambi.
Alisema ushindi huo umerejesha hali ya kujiamini kwa timu hiyo hasa kwa ushindi wa mabao mengi walioupata akiamini sasa wameanza kurejea mchezoni na wanapaswa kujipambanua kutoka kwenye nafasi waliyo sasa na kupanda juu zaidi katika msimamo.
Namungo imepata ushindi huo ikiwa ni mechi ya kwanza kushuka dimbani bila ya aliyekuwa kocha wao, Cedric Kaze aliyetangaza kujiuzulu siku sita zilizopita.