Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema licha ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Singida Fountain Gate lakini ameeleza kufurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake kilichotoa taswira nzuri kwenye michezo ijayo.
Matokeo ya mchezo huo wa raundi ya saba uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam umeifanya Yanga kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC ikifikisha pointi 18 dhidi ya Simba SC inayoshika nafasi ya pili ikiwa pia na pointi 18.
Gamondi alisema ulikuwa mchezo mgumu ambao kila timu ilihitaji kupata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri, ila amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake ambao wameendelea kuwa kwenye ubora licha ya kucheza michezo migumu mfululizo.
“Tumecheza michezo miwili migumu mfululizo na kupata ushindi, malengo yetu ni kutetea ubingwa hivyo tunahitaji wachezaji ambao wako timamu wakati wote ambao watakuwa tayari kuipambania timu, nimeona baadhi ya wachezaji wameimarika tayari kupigania namba,” alisema Gamondi.
Alisema wanamchezo mgumu dhidi ya Simba ambao utachezwa Novemba 5, mwaka huu anaamini watafanya vizuri kutokana na kila mchezaji kuutaka mchezo huo.
Alisisitiza kuwa maandalizi ya kila mchezo wanajiandaa kulingana na mpinzani ambaye wanakwenda kukutana naye, hivyo maandalizi ya Simba wanatakiwa kuongeza umakini zaidi kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Ingawa ni mapema sana kuanza kuizungumzia Simba, lakini ndio mchezo unaofuata, kila mchezaji anaonesha juhudi tunapokuwa mazoezini kwa ajili ya kupambania nafasi ya kucheza dhidi ya Simba,” alisema Gamondi.
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Ricardo Fereira, alisema walihitaji nguvu ya ziada kwenye mchezo dhidi ya Yanga ili wapate ushindi kwani walifanya maandalizi mazuri kwa wiki nzima lakini wameshindwa kuondoka na pointi tatu.
“Nimeona kuna baadhi ya maeneo ya kuyafanyia maboresho kiufundi na kwenye utimamu lakini wachezaji walipambana kufanya kitu ili kupata matokeo, dakika 20 hadi 25 tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa lakini baada ya kufungwa bao akili yetu ikabadilika tukaanza kucheza kwa presha,” alisema Fereira.
Kila lakheri Yanga