Madrid, Hispania
Kocha Carlo Ancelotti ameshangazwa na kiwango cha ufungaji mabao cha kiungo Jude Bellingham baada ya mchezaji huyo kufunga mabao mawili Real Madrid ikiwalaza mahasimu wao, Barcelona mabao 2-1.
Bellingham kwanza alifunga bao la kusawazisha dakika 68 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Olympic baada ya Ilkay Gundogan kuipa Barca bao la kuongoza mapema dakika ya sita.
Kiungo huyo wa England aliongeza bao la pili kwa timu yake katika dakika za nyongeza na kuifanya Real Madrid itoke na pointi tatu muhimu zinazoifanya ishike usukani wa La Liga ikiwa na pointi 28.
“Kwanza alifunga bao lililovutia akawa makini hadi kufunga bao la pili, tunashangazwa, kila mmoja anashangazwa na kiwango chake hasa kiwango cha umakini akiwa mbele,” alisema Ancelotti baada ya mechi hiyo.
“Anaingia kwenye ‘boksi’ lakini leo shuti la bao la kwanza limetushangaza, amefunga bao ambalo limekuwa kivutio mno, kwa sasa ni aina ya mchezaji anayeweza kuleta utofauti,” alisema Ancelotti.
Bellingham kwa sasa amefikisha mabao 10 katika mechi 10 za ligi akiwa kwenye msimu wake wa kwanza na Real Madrid na ndiye kinara wa mabao na kwa mashindano yote hadi sasa ana mabao 13 baada ya kufunga matatu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Anaonekana kama ni mchezaji mkongwe, yuko vizuri, bao lake la kusawazisha lilibadili kabisa kasi ya mchezo, lilimaanisha sisi kupata nguvu zaidi na kusababisha udhaifu kwa Barcelona ambao tayari walikuwa wanacheza vizuri hadi wakati huo,” aliongeza Ancelotti.
Bellingham pia alisifiwa na kiungo mwenzake wa timu hiyo, Luka Modric ambaye alisema kwamba wanamfurahia mchezaji huyo na kuongeza kuwa kwa sasa anaonekana kama amekuwa kwenye timu hiyo kwa kipindi kirefu.
Matokeo mechi za La Liga Jumamosi…
Barcelona 1-2 Real Madrid
Almería 1-2 Las Palmas
Mallorca 0-0 Getafe
Cadiz 2-2 Sevilla