Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeingia kambini leo Alhamisi asubuhi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Ihefu ikitamba kuwa itaibuka na ushindi kwa kuwa timu hiyo haijawahi kuwasumbua.
Simba ambayo imerejea jana ikitokea Cairo ilikotolewa kwenye michuano ya African Football League na Al Ahly ya Misri imejinasibu kuelekeza nguvu zote katika mchezo huo na kuendeleza wimbi lake la ushindi mfululizo wa mechi za ligi.
Akizungumza na GreenSports, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kocha wao Roberto Oliveira au Robertinho anatambua kuwa Ihefu haijawahi kuwasumbua kama inavyofanya kwa wengine, hivyo anaiandaa timu kwa ajili ya kuendelea walipoishia.
“Upande wetu Ihefu haijawahi kutusumbua, msimu uliopita tumeifunga nyumbani na ugenini na sasa timu imeingia kambini kujiandaa vizuri zaidi kuhakikisha tunaliendeleza hilo na kwa bahati nzuri hakuna majeruhi, hivyo kila kitu kinakwendw vizuri,” alisema Ally.
Meneja huyo pia alisema kwamba japokuwa Ihefu ina kocha mpya kwa sasa, Moses Basena raia wa Uganda, lakini hawatishiki na hilo kwani wako tayari kukutana na falsafa yoyote na kupambana nayo.
Simba ambayo imeshinda mechi tano mfululizo za ligi msimu huu mpaka sasa, msimu uliopita iliifunga Ihefu nyumbani na ugenini na kuweka rekodi ya kuifunga timu hiyo mechi zote walizokutana kwenye Ligi Kuu NBC.