Na mwandishi wetu
Kipa namba moja wa Azam FC, Abdulai Iddrisu amewaomba radhi wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kwa makosa yaliyosababisha wafungwe na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliofanyika Uwanja wa Mkapa juzi Jumatatu.
Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2, mabao yote ya Yanga yakifungwa na Stephane Aziz Ki.
Kipa huyo raia wa Ghana alisema makosa yake ndio yamesababisha wasipate pointi tatu muhimu ambazo zingewaweka kileleni mwa msimamo wa ligi na kuwa na mwenendo mzuri wa kutofungwa tangu msimu huu uanze.
“Bao la kusawazisha la Yanga, lilitokana na makosa yangu ndio liliwapa wapinzani nguvu ya kurudi mchezoni na kufunga bao la ushindi, naomba msamaha kwa viongozi, wachezaji wenzangu na mashabiki wa Azam FC ilikuwa ni tukio ambalo sikulitegemea,” alisema Iddrisu.
Kipa huyo alisema wakati anaingia kwenye mchezo huo alipania kuipigania timu yake kupata ushindi na baada ya wao kuwa mbele kwa mabao 2-1 aliamini ni muda wa kulinda walichokuwa nacho lakini kilichomtokea hadi kufanya makosa hayo kilimshangaza na kumuumiza .
Alisema tukio lile bado linamuumiza kila linapomjia kichwani lakini atahakikisha analifanyia kazi ili lisije kujirudia tena hasa kwenye mechi kubwa kama ile.
Iddrisu alisajiliwa na Azam kwenye dirisha dogo msimu uliopita, kutoka Becham United ya Ghana, lengo likiwa ni kumpa upinzani aliyekuwa kipa namba moja wakati huo Ali Ahmada raia wa Comoro ambaye naye alikuwa na makosa mengi ya kiufundi.