Na mwandishi wetu
Bondia Ibrahim Mgenda maarufu Ibra Class amesema amejipanga vizuri kumvaa Xiao Su wa China katika pambano la kuwania mkanda wa TPBC litakalofanyika keshokutwa Jumamosi kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam. Akizungumza leo Alhamisi jijini Dar es Salaam, Class alisema anajua ugumu wa mpinzani wake lakini hamhofii kwani amefanya maandalizi ya muda mrefu na kipigo kitakuwa pale pale, tayari kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania. “Nimefanya maandalizi mazuri katika kambi niliyoiweka mkoani Tanga na niko tayari kuwasha moto, namwambia Mchina kuwa hatoki salama lazima aondoke na kovu nitakalompa,” alisema Class. Class hajapoteza pambano lolote hivi karibuni, kiwango chake kikionekana kupanda kadri siku zinavyokwenda. Ni bondia anayeshika nafasi ya kwanza Tanzania katika uzito wa ‘super featherweight’ akiwa na nyota mbili na nusu. Amecheza mapambano 36 akiwa ameshinda 30 na kupoteza sita. Kwa upande wa mpinzani wake kutoka China, bondia huyo amecheza mapambano 15 na kati ya hayo, ameshinda 12 na kupoteza matatu.