Na mwandishi wetu
Aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Crecentius Magori amesema ili wafanikiwe kuitoa Al Ahly, wachezaji wanatakiwa kujitoa zaidi ya dakika 90 za Uwanja wa Mkapa ingawa haitokuwa mechi rahisi kwao.
Simba itaumana na Ahly leo Jumanne katika mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika Football League (AFL), mechi ambayo Simba itakuwa ikiwania kutinga nusu fainali iwapo itaishinda Al Ahly.
Magori alisema kuwa Simba inataka kuandika historia mpya barani Afrika na ili ifanye hivyo inapaswa kuiondoa kwanza Al Ahly, ambao ndio vigogo tishio zaidi.
“Simba tuna wakati mgumu sana katika mchezo wa marudiano na Al Ahly na wala tusijidanganye, inabidi wachezaji wakafanye kazi zaidi na kujitolea ingawa hakuna kinachoshindikana,” alisema Magori.
“Shida yetu kubwa ni namna ambavyo timu inacheza isipokuwa na mpira, hatukabi kwa ufanisi, ndio maana unaona timu yetu imeruhusu mabao katika michezo mingi tuliyocheza,” alisema Magori.
Alisema ili kucheza na timu aina ya Al Ahly wachezaji wanapaswa kukimbia mara mbili zaidi, kufanya kazi maradufu zaidi na kumwaga jasho, kuwa bora zaidi ya kawaida kwa kuwa wao tayari wako bora.
Simba itashuka Uwanja wa Cairo mjini Cairo katika mchezo wa marudiano baada ya ule wa awali uliochezwa Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira alisema: “Nafahamu tutakuwa na mechi ngumu dhidi ya timu kubwa Afrika ila kuna namna ambavyo tutaingia na mpango tofauti na ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza nyumbani.
“Tunawaheshimu Al Ahly ni timu kubwa yenye mashabiki wengi lakini zimebaki dakika 90 ambazo zitaamua nani anasonga mbele, nimewaambia vijana wangu wasahau matokeo yaliyopita akili na nguvu wahamishie kwenye mchezo wa leo.”
Kocha huyo Mbrazili alisema atakuwa na mabadiliko ya wachezaji kwenye baadhi ya maeneo ili kufanikiwa kucheza vizuri zaidi na kupata ushindi ili watinge hatua inayofuata ya nusu fainali ya michuano hiyo inayochezwa kwa mara ya kwanza Afrika.