Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema ameanza kuziona dalili za kubeba ubingwa kufuatia kiwango bora ambacho kimeoneshwa na timu yake katika mchezo wa jana Jumatatu dhidi ya Azam FC.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, mabingwa watetezi Yanga ilishinda kwa mabao 3-2 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC wakifikisha pointi 15 sawa na Simba lakini mabingwa hao watetezi wapo mbele kwa mchezo mmoja.
Gamondi alieleza kuwa wachezaji wake walionesha tabia halisi za timu bingwa na wanahitaji ubingwa msimu huu kutokana na kucheza kwa kujitoa na kutafuta pointi tatu licha ya kutanguliwa.
“Nilitarajia ugumu kwenye mchezo huo, wachezaji wangu wameonesha tabia halisi ya kwamba wapo kwenye timu kubwa inayohitaji ubingwa, tulicheza vizuri kipindi cha pili licha ya kutanguliwa bao la penalti lakini tulipambana na kusawazisha makosa yetu,” alisema Gamondi.
Kocha huyo pia alimpongeza mfungaji wa mabao yote matatu Stephane Aziz Ki, akisema ni mchezaji wa daraja la juu mno na pamoja na uchovu aliokuwa nao lakini alicheza kwa kujitoa kuipigania timu, kitu ambacho kimeonesha ana mapenzi makubwa na klabu hiyo.
Naye Kocha Msaidizi wa Azam, Bruno Ferry alisema kilichowaangusha ni kushindwa kudhibiti mchezo baada ya kuongoza kwa mabao 2-1 kutokana na kukosa uzoefu kwa baadhi ya wachezaji wake.
Alisema ulikuwa mchezo mkubwa uliokutanisha timu mbili kubwa na walijitahidi kupambana kwa kuushika mchezo katika baadhi ya nyakati lakini ubora wa Yanga hasa kiungo Aziz Ki ndio uliowaletea shida na kujikuta wanapoteza mchezo.
“Naipongeza Yanga pamoja na Aziz Ki, alikuwa bora na ndio amesababisha tukapoteza mchezo lakini ndio mpira tunarudi kujipanga ili kufanya vizuri mchezo unaokuja lengo ni kubeba ubingwa wa ligi kuu msimu huu,” alisema Ferry.
Jamani ligi bado mbichi hivi mnaandikia habari zenu ushaki eheeeeeeeee.