Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga umetamba kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC unaotarajia kupigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar Es Salaam, Jumanne ijayo.
Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison alisema wanaingia kwenye mchezo huo lengo lao kubwa likiwa ni kuondoka na pointi tatu zitakazowarudisha kileleni mwa msimamo wa ligi kutoka nafasi ya tatu waliyopo sasa.
“Maandalizi yetu yanaendelea kwa umakini mkubwa sababu huu ni mchezo mkubwa ambao tunatarajia utakuwa na upinzani mkali kutokana na ubora wa timu zote mbili lakini tumejipanga kuendeleza furaha,” alisema Walter.
Meneja huyo alieleza kuwa kila mchezaji kwenye kambi yao ameonesha utayari mkubwa kuelekea mchezo huo na dhamira yao ni kuhakikisha wanaendeleza machungu kama ilivyokuwa kwenye mechi zilizopita.
Alisema kocha wao mkuu, Miguel Gamondi amekuwa akitumia siku zilizobaki kuwapa wachezaji wake mbinu muhimu ambazo zitasaidia kuwapa ushindi katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini.
Wakati Yanga wakijitapa kuendeleza machungu kwa wapinzani wao Azam, kocha mkuu wa timu hiyo, Youssouf Dabo alisema safari hii hayupo tayari kuona wakipoteza mchezo dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC.
“Tupo tayari kucheza na Yanga katika uwanja wowote, tumeimarika kuliko wanavyofikiria, tunajua madhaifu yao mengi ambayo nimewaelekeza vijana wangu hivyo wajipange kutukabili,” alisema Dabo raia wa Senegal.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa sasa kila shabiki wa soka anasubiri kwa hamu kuona kwenye mechi hii ya kwanza ya ligi nini kitatokea baada ya kila timu kujinadi kujipanga vilivyo.