Roma, Italia
Kocha wa Roma, Jose Mourinho amepewa kadi nyekundu kwa kuwadhihaki wapinzani wao Monza kwa kujifanya analia mbele ya benchi la timu hiyo baada ya Roma kupata bao pekee na la ushindi katika mechi baina ya timu hizo.
Bao hilo pekee linaifanya Roma kufikisha pointi 14 kwenye lgi ya Serie A ingawa kwa kocha huyo kadi aliyopewa ni mwendelezo wa adhabu ambazo amekuwa akikumbana nazo akiwa na rekodi ya kuadhibiwa mara tatu kwa makosa tofauti tofauti msimu uliopita.
Stephan El Shaarawy ndiye aliyefunga bao hilo pekee la Roma katika dakika ya 90 baada ya timu hiyo kushindwa kuzitumia nafasi mbili kupitia Romelu Lukaku na Sardar Azmoun ambao mashuti yao yaligonga mwamba.
Monza katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumapili walilazimika kucheza 10 uwanjani kwa takriban dakika 50 baada ya Danilo D’Ambrosio kupewa kadi nyekundu dakika tano kabla ya kipindi cha kwanza.
Ushindi huo wa Roma umeivuruga rekodi nzuri ya ushindi wa Monza ambayo haikupoteza mechi hata moja kati ya tano zilizopita.
“Sijui ni kwa nini nimepewa kadi nyekundu, nilichofanya ni kutoa ishara kwenye benchi la Monza na sikutamka neno lolote,” alisema Mourinho.
“Tulifanya makosa mengi na yalituumiza, ilikuwa mechi yenye ufundi wa chini mno badala yake ilijaa mihemko,” aliongeza kocha huyo.
Matokeo ya mechi za Serie A wikiendi…
Roma 1-0 Monza
AC Milan 0-1 Juventus
Bologna 2-1 Frosinone
Salernitana 2-2 Cagliari
Atalanta 2-0 Genoa