Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema amewaona Al Ahly ya Misri na atahakikisha anaandaa mbinu bora za kuwakabili ili kupata ushindi katika mechi hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi alikuwa miongoni mwa walioushuhudia mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Football League (AFL) kati ya Simba na Al Ahly uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, kocha huyo raia wa Argentia alisema hana mengi ya kuongea kuhusu wapinzani wake hao isipokuwa atatumia siku zilizobaki kukiimarisha kikosi chake ili waweze kukabiliana nao katika mechi zote mbili.
“Nimewaona Al Ahly ni timu kubwa na bora Afrika, wana wachezaji wenye uwezo na uzoefu mkubwa lakini vipo vitu nimeviona tunakwenda kuvifanyia kazi kwa ajili ya kuvitumia kwenye mchezo wetu wa hatua ya makundi,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema mpira ni mchezo wa mbinu ambao unabadilika kila kukicha hivyo ni vigumu kuyafanyia kazi moja kwa moja mapungufu waliyoonesha Al Ahly katika mchezo wa juzi sababu wanaweza kuja kivingine na wao wakajikuta wanashindwa kuwakabili.
Alisema atakachofanya ni kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya kushindana na timu kubwa Afrika na siyo kufuata moja kwa moja kile alichokiona kwenye mchezo wa Ahly na Simba.
Mbali na Al Ahly timu nyingine zilizopo kwenye kundi la Yanga ni RC Belouzdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.