Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza amesema matokeo waliyoyapata dhidi ya Al Ahly ya Misri si mazuri sana na sasa wanajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mechi ya marudiano.
Wekundu hao walipata sare ya mabao 2-2 jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League (AFL) inayoshirikisha timu nane za Afrika.
Saido aliyetoa pasi ya bao la pili la Simba alisema wana furaha kwa matokeo hayo lakini si waliyokuwa wakiyataka kwani ushindi ndio muhimu zaidi japo anawapongeza wachezaji wenzake kwa namna walivyojitoa kupambana katika mchezo huo.
“Al Ahly ni timu kubwa na tunashukuru Mungu kwa matokeo haya, huu ni mchezo wa kwanza na sasa tunasubiri wa pili kuona tutafanya nini lakini binafsi nawapongeza kila mchezaji, kila mmoja alipambana, hii ni sare ya 2-2 lakini kwenye mpira lolote linatokea, tusubiri mechi ya pili,” alisema Saido.
Alisema kwa sasa wanakubaliana na matokeo hayo lakini wanakwenda kujipanga zaidi wakitambua mchezo wa ugenini hautakuwa mwepesi, akiamini kocha wao Roberto Oliveira ‘Robertinho’ atakuwa na mbinu za kuwavuruga wapinzani wao nyumbani kwao.
Timu hizo zinatarajia kurudiana keshokutwa Jumanne kwenye Uwanja wa Cairo uliopo mjini Cairo huku Simba ikihitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Kimataifa Saido hajayafurahia matokeo na Ahly
Saido hajayafurahia matokeo na Ahly
Read also