Liverpool, England
Mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah ametaka viongozi duniani kote kukaa pamoja ili kuzuia mauaji ya raia wasio na hatia yanayoendelea katika mzozo wa Israel-Gaza.
Taarifa za maofisa wa afya zimeeleza kuwa maelfu ya watu wa Palestina wameuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika hospitali moja katika mji ya Gaza juzi Jumanne usiku.
Salah alisema kwamba ukatili na matukio ya umwagaji damu vimeongezeka huku akitaka misaada ya kibinadamu iruhusiwe kuwafikia wahanga wa machafuko hayo.
Maofisa wa Palestina walisema kwamba mlipuko huo wa bomu katika Hospitali ya Al-Ahli Arab ulitokana na uvamizi wa kutumia mabomu ya anga uliofanywa na Jeshi la Anga la Israel.
Taarifa za kijeshi za Israel hata hivyo zilidai kwamba mlipuko huo ni matokeo ya roketi iliyoshindwa kufanya kazi vizuri ambayo ilirushwa na kikundi cha Islamic Jihad cha Palestina, kauli ambayo imepingwa na kikundi hicho.
Ndege za kijeshi za Israel zimekuwa zikirusha mabomu katika maeneo ya Gaza ikiwa ni kujibu mapigo baada ya uvamizi uliofanywa Oktoba 7 na kundi la Hamas la Palestina na kusababisha vifo vya watu 1,400.
Akizungumzia matukio hayo kupitia video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, Salah alisema kwamba inasikitisha, “Mazingira katika hospitali yanasikitisha, watu wa Gaza wanahitaji chakula, maji na huduma za matibabu kwa haraka.”
“Nawasihi viongozi duniani kote kukaa pamoja ili kuzuia mauaji zaidi ya mioyo ya watu wasio na hatia, maisha ya watu lazima yalindwe, mauaji yanahitaji kukomeshwa, familia zimetenganishwa,” alisema Salah.
Shirikisho la Soka Algeria jana Jumatano lilitangaza kuahirisha mechi za mashindano ya soka nchini humo kwa nia ya kuwaunga mkono watu wa Palestina na kukubali timu ya Palestina kuweka kambi Algeria na kutumia viwanja vya nchini humo kwa mechi zao.