Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia, Neymar atalazimika kufanyiwa upasuaji baada ya kuumia misuli ya goti la mguu wa kushoto wakati akiiwakilisha Brazil.
Neymar aliuamia juzi Jumanne katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Uruguay, mechi ambayo Brazil ililala kwa mabao 2-0 na mchezaji huyo kutolewa uwanjani akiwa amebebwa kwenye machela.
Mara baada ya kuumia katika dakika ya 44, Neymar alilala chini na baadaye alinukuliwa kupitia mitandao ya kijamii akisema kwamba kimekuwa kipindi kigumu mno kwake. “Najua niko imara lakini safari hii nitaihitaji zaidi familia yangu pamoja na marafiki.”
Haijaweza kufahamika mara moja muda ambao Neymar atautumia hadi kupona ingawa katika hali ya kawaida kwa aina ya upasuaji atakaofanyiwa atahitaji kipindi cha kuanzia miezi minane hadi 10.
“Watu wa Brazil na dunia ya watu wa soka wanamhitaji Neymar akiwa mwenye afya na aliyepona kwa sababu soka inakuwa raha Neymar anapokuwa uwanjani,” alisema rais wa Shirikisho la Soka Brazil, Ednaldo Rodrigues katika taarifa yake.
Neymar, 31 kwa sasa anashika namba moja kwa kuifungia mabao mengi timu ya taifa ya Brazil, aliihama PSG ya Ufaransa mwishoni mwa msimu uliopita na kujiunga na Al-Hilal ingawa kwa miaka ya karibuni amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
“Si jambo rahisi kupitia majeraha na upasuaji, jaribu kufikiri unarudia jambo hilo kwa mara nyingine baada ya miezi minne ya kuwa fiti,” alisema Neymar.