Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso aliyepigwa busu la mdomoni na aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania (RFEF), Luis Rubiales, hatimaye ameitwa timu ya taifa.
Tukio la Jenni kupigwa busu Agosti 20 baada ya Hispania kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) lilizua taharuki na kusababisha kujiuzulu kwa Rubiales katika nafasi ya urais wa RFEF.
Jenni awali alinukuliwa akisema kwamba hakulipenda jambo hilo kwa madai kwamba hakukuwa na makubaliano yoyote baina yao na kuahidi kuchukua hatua za kisheria.
Hispania itaumana na Switzerland baadaye mwezi huu katika mechi ya Nations Ligi na kuitwa kwa Jenni kumekuja baada ya mchezaji huyo kuachwa katika kikosi kilichochaguliwa mwezi uliopita kwa kilichoelezwa kuwa ni kwa ajili ya kumlinda.
Wakati kocha mpya wa Hispania, Montse Tome akitangaza kikosi cha timu hiyo alisema kwamba awali waliona ni muhimu kutompa nafasi Jenni katika timu hiyo ili kumlinda na kilichokuwa kikiendelea kwa wakati huo.
Alisema kwamba walimuarifu sababu za kutomchagua katika timu iliyopita lakini kwa sasa wameona mabadiliko na wana furaha kuwa naye katika timu hiyo kwa mara nyingine.
Kocha aliyeiwezesha Hispania kubeba Kombe la Dunia, Jorge Vilda naye alitimuliwa mwezi uliopita na anachunguzwa akidaiwa kuwa mmoja wa wahusika katika tuhuma za kijinai zinazomkabili Rubiales.
Rubiales ambaye pia alifungiwa na Fifa kujihusisha na soka kwa siku 90 kabla ya kutangaza kujiuzulu katika nafasi ya urais wa RFEF, amekana mahakamani kufanya kosa lolote ikiwamo udhalilishaji kijinsia dhidi ya Jenni na amepewa amri ya kutomsogelea mchezaji huyo kwa umbali wa mita 200.
Kimataifa Aliyepigwa busu aitwa timu ya taifa Hispania
Aliyepigwa busu aitwa timu ya taifa Hispania
Read also