Na mwandishi wetu
Timu ya Azam FC imeeleza kuwa inaamini huu ni msimu wao wa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu NBC kutokana na hali walizonazo wapinzani wanaochuana nao kwenye vita hiyo.
Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe ameiambia GreenSports leo Jumatatu kuwa kwanza wapo nyuma ya kinara wa ligi kwa pointi mbili lakini kingine timu yao haina presha kama zilivyo Simba na Yanga ambazo nazo zinapigiwa chapuo kuendelea kutawala ligi hiyo msimu huu pia.
Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 13, Simba inaongoza kwa pointi 15 huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi 12 baada ya kila timu kucheza mechi tano.
“Ni tofauti ya pointi mbili, aliye juu hayuko mbali lakini nafikiri tuna sababu ya kujivunia kama timu hapa tulipo maana nasi ni washindani wa kombe kwa sasa na sababu tunazo maana tuna kocha mgeni (Youssouph Dabo) anapata ujuzi kwa mara ya kwanza ligi ya hapa na amefanya kazi nzuri mpaka sasa.
“Kwa sababu kocha anataka kuonesha kitu lakini wenzetu wanajiamini zaidi kwamba wanastahili kutwaa ubingwa na hiyo inakupa presha ya juu kwamba ni lazima ufanye hivyo, sasa sisi hatuna hiyo, tunachojua tuna timu nzuri na tunashindania ubingwa,” alisema Ibwe.
Azam iliyoanza kushiriki ligi kuu msimu wa 2008-09 inatazamia kutwaa ubingwa huo iweke rekodi ya kutwaa mara ya pili baada ya kufanya hivyo msimu wa 2013-14 bila kufungwa mechi yoyote ya ligi.