Na mwandishi wetu
Wawakilishi wa Tanzania kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, timu ya JKT Queens watatupa karata yao ya kwanza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Novemba 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hiyo itakuwa ni mechi ya pili ya ufunguzi wa fainali hizo itakayochezwa kuanzia saa 11.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Mechi ya kwanza itakuwa kati ya wenyeji wa fainali hizo Athlético d’Abidjan ya Ivory Coast dhidi ya SC Casablanca ya Morocco saa 8.00 mchana na kukamilisha mechi za kwanza za Kundi A.
JKT itashuka dimbani kwa mchezo wa pili dhidi ya Abidjan, Novemba 8 majira ya saa 8.00 mchana kisha itamaliza mchezo wake wa tatu hatua ya makundi kwa kupepetana na SC Casablanca, mechi itakayopigwa Novemba 11 kuanzia saa 12.00 jioni.
Mshindi wa kwanza Kundi A atacheza na mshindi wa pili wa Kundi B katika nusu fainali ya kwanza na nusu fainali ya pili atacheza mshindi wa kwanza Kundi B na mshindi wa pili Kundi A.
Nusu fainali zitapigwa Novemba 15 kabla ya fainali Novemba 19, mwaka huu. Kundi B linaundwa na timu za Ampem Darkoa ya Ghana, Huracanes (Guinea ya Ikweta), AS Mande (Mali) na mabingwa watetezi, AS FAR ya Morocco.
Fainali hizo zinafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake ambapo bingwa anatarajia kunyakua Dola za Marekani 400,000 (sawa na Sh milioni 998), mashindi wa pili Dola 250,000.
Timu zitakazoishia nusu fainali zitachota Dola 200,000 wakati watakaomaliza wa tatu katika kundi watazoa Dola 150,000 na wa nne ataondoka na Dola 100,000.
JKT Queens ilipata nafasi ya kushiriki fainali hizo baada ya kuibuka kinara na kubeba taji la ukanda wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Soka JKT Queens kuanza na Mamelodi Ligi ya Mabingwa
JKT Queens kuanza na Mamelodi Ligi ya Mabingwa
1 Comment
Leave a Reply Cancel reply
Read also
Mwaka huu vipi Simba Qeen haikupata nafasi?