London, England
Kiungo wa England, Jordan Henderson ameamua kuwapuuza mashabiki wa England waliomzomea katika mechi yao na Australia akisema amepokea zomea zomea hiyo na ataendelea kuichezea timu hiyo kadri awezavyo.
Henderson, nyota wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ettifaq ya Saudi Arabia alijikuta akizomewa na mashabiki wa England katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Wembley na England kushinda kwa bao 1-0.
Kiungo huyo ambaye alikuwa nahodha wa England katika mechi hiyo alikutana na zomea zomea hiyo ya mashabiki hata wakati akitolewa katika dakika ya 62 ya mchezo huo uliochezwa Ijumaa iliyopita.
“Si jambo zuri mashabiki wako kukuzomea, napenda kuichezea England, nimekuwa nikifanya hivyo kwa miaka mingi na ndio maana bado niko hapa, na shutuma zao nimezipokea,” alisema Henderson.
Henderson, 33, ambaye amekuwa nahodha wa England katika mechi 79 alisisitiza kwamba anapenda kuichezea England, “napenda kuichezea England kwa muda mrefu kadri iwezekanavyo na kujitolea kwa ajili ya timu, kwa ajili ya nchi yangu.”
“Kila mtu ana maoni yake kuhusu mimi kucheza Saudi Arabia, nimezungumza hili huko nyuma kuhusu sababu za uamuzi huo kama watu wanakubali au hawakubali ni juu yao, ninachofanyiwa kinanisikitisha lakini hakiwezi kubadili ninachofanya hapa, nataka kuendelea kucheza na kupambana na kuisaidia timu iwe na mafanikio,” alisema Henderson.
Awali Henderson alidaiwa kuwa mtetezi wa makundi yanayojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wakati akiwa Liverpool, baadaye alishutumiwa kwa kukubali kuhamia Saudi Arabia nchi ambayo mapenzi ya jinsia moja ni haramu.
Kwa upande wake kocha wa England, Gareth Southgate alisema zomea zomea ya mashabiki kwa Henderson inakosa mantiki na haitarajiwi kwa mchezaji anayejitolea kwa moyo wake kuichezea England.
England kesho Jumanne itakuwa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2024 (Euro 2024) dhidi ya Italia, mechi itakayopigwa kwenye dimba la Wembley.