Na mwandishi wetu
Wachezaji wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, wamezizungumia timu za Morocco, DR Congo na Zambia walizopangwa nazo kundi moja kwenye kwenye fainali za Afcon ambapo licha ya kukiri kuna ugumu lakini wanaamini hakuna kinachoshindikana.
Wakizungumza katika mahojiano yao wakiwa Saudi Arabia walikoenda jana Ijumaa kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan, kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya alisema hawawahofii wapinzani wao.
Akifafanua zaidi Kakolanya alisema kwamba wanawaheshimu wapinzani hao huku akisisitiza kuwa wanajipanga vilivyo kuhakikisha safari hii wanaibuka hatua ya makundi.
“Kundi siyo jepesi ni gumu na kila mtu ameliona, kwa upande wetu tutapambana kuhakikisha sasa hivi tunavuka kwenda robo fainali, nafikiri maombi ya Watanzania yawe makubwa sana safari hii.
“Hatuwaogopi wapinzani, tunawaheshimu na nafikiri na wao pia waje kwa kutuheshimu maana huu ni muda tunaohitaji matokeo na kocha (Adel Amrouche) ameliona hilo, naamini anajua maandalizi yanaendaje, anatakiwa tuwe vipi,” alisema Kakolanya.
Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta alisema ingawa wamepangwa Kundi F wakitokea chungu namba nne, hiyo ina maana kubwa kuelekea michuano hiyo dhidi ya vigogo hao, akiamini soka la Afrika halitabiriki na lolote linaweza kutokea endapo watajipangaza vizuri kuanzia sasa.
Naye beki Novatus Dismas alisema: “Siwezi kuwazungumzia sana wapinzani, kila mmoja anajiandaa kivyake, majina ya timu tunazokutana nazo ni makubwa lakini naamini tunaweza kufanya kitu kikubwa zaidi ya majina yao, nafikiri tuna kikosi kizuri na bado tunatengeneza timu na kocha pia ni mgeni hivyo tunahitaji muda mwingi wa kuwa pamoja.”
Mshambuliaji Simon Msuva alisema ingawa wana uzoefu mdogo wa ushiriki wa michuano hiyo lakini watajiandaa vizuri kwa kutumia uzoefu walionao huku wakikazania kufanya maandalizi kabambe ili kufikia ndoto walizonazo katika michuano hiyo itakayofanyika Ivory Coast, mwakani.
Naye beki Dickson Job alisema uwepo wa baadhi ya wachezaji wa DR Congo na Zambia katika Ligi Kuu NBC, anaamini watatumia kama faida katika kujipanga juu ya wapinzani wao hao kuhakikisha wanafanya vizuri dhidi yao.
Stars imerejea kwenye michuano hiyo inayoshiriki kwa mara ya tatu baada ya kushiriki mwaka 1980 na 2019 huku sasa ikitaka kuweka reodi kwa kuvuka hatua za mbele zaidi baada ya mara zote kuishia hatua ya makundi.