London, England
Kocha Birmingham Wayne Rooney alikataa ofa ya kwenda kufanya kazi Saudi Arabia kwenye ligi kuu ya nchini humo ‘Saudi Pro Ligi’ na kuchagua kurudi England kuinoa timu hiyo inayoshiriki ligi ya Championship.
Rooney, mshambuliaji wa zamani wa klabu za Man United, Everton na timu ya taifa ya England, hivi karibuni aliachana na timu ya D.C United ya Marekani na Jumatano iliyopita alitangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa Birmingham.
Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Birmingham, Garry Cook alisema kwamba alijaribu kumshawishi Rooney aende Saudi Arabia wakati yeye akiwa CEO wa Saudi Pro Ligi lakini jambo hilo halikufanikiwa.
Kama Rooney angekubali kwenda kufundisha timu Saudi Arabia, angekuwa anaungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa timu ya England, Steven Gerrard ambaye kwa sasa anainoa timu ya Al-Ettifaq ya Saudi Arabia.
Rooney alisema kwamba uamuzi wake wa kukataa kwenda Saudi Arabia haumaanishi kuwakosea heshima makocha waliochagua kwenda huko badala yake alisema uamuzi huo ni wake binafsi ambao umezingatia mendeleo yake na njia tofauti aliyoichagua.
“Nilijifikiria mimi na kuamua kurudi katika soka la England ni jambo zuri, ni jambo ambalo nimekuwa nikitaka kulifanya, katika wiki nne au sita zilizopita nilikuwa na ofa katika klabu nyingine lakini tangu nizungumze na Birmingham, uamuzi ulikuwa rahisi,” alisema Rooney.
Birmingham kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenda Championship na mechi ya kwanza ya Rooney akiwa na timu hiyo itakuwa Oktoba 21 dhidi ya Middlesbrough.