Rio de Janeiro, Brazil
Kocha wa Brazil, Fernando Diniz amechukizwa na kitendo cha mashabiki wa timu hiyo kumpiga kichwani na mfuko wa bisi mshambuliaji wa timu hiyo, Neymar katika mechi dhidi ya Venezuela iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Mfuko huo wa bisi au popcorn ulirushwa wakati Neymar akitoka katika dimba la Pantanal mara baada ya mechi hiyo ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 iliyochezwa juzi Alhamisi.
Neymar ambaye alicheza mechi hiyo dakika zote baada ya tukio hilo kocha wake alijaribu kumlinda na mchezaji huyo alionekana akiwatolea maneno makali mashabiki waliokuwa eneo ambalo mfuko huo wa bisi ulitokea.
“Hakika sikubaliani na hili, kumzomea na kumshutumu mchezaji sina tatizo lakini kurusha mfuko wa bisi hakumsaidii mtu, ni ukosefu wa heshima kwa wachezaji waliokuja hapa kucheza na kujitahidi kadri walivyoweza,” alisema Diniz.

Diniz pia alionesha kukerwa kwa namna ambavyo Brazil ilishindwa kupata ushindi na hivyo kujikuta ikizidiwa na Argentina walioifunga Paraguay bao 1-0 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa kuwa na pointi mbili zaidi ya Brazil baada ya kucheza mechi tatu.
“Tungeweza kupata bao la pili, la tatu na la nne, tulimalizia uchezaji wetu vibaya, na pia tusingeruhusu kufungwa goli na Venezuela, tungekuwa makini katika kukaba na kutowapa wapinzani nafasi ya kumalizia,” alisema Diniz.
Katika mechi hiyo, Neymar ndiye aliyetoa pasi ya kona iliyozaa bao la Brazil lililofungwa na beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes kabla Venezuela hawajasawazisha kupitia Eduard Bello jambo lililowakera mashabiki wa Brazil waliotaka kuona timu yao ikipata ushindi wa tatu mfululizo.
Brazil itajitupa tena uwajani Jumanne ijayo ugenini kwa kuumana na Uruguay, mechi ambayo itapigwa mjini Montevideo.