Na mwandishi wetu
Aliyekuwa kocha mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila amesema anaitakia kila la kheri timu hiyo, akiitaka iendeleze umoja na ipambane kufikia malengo yake hata baada ya yeye kuondolewa katika kikosi hicho.
Katwila ameeleza hayo leo Jumamosi akizungumza na GreenSports muda mfupi baada ya Ihefu FC kutangaza kuachana naye baada ya kuiongoza katika mechi tano za Ligi Kuu NBC msimu huu.
“Siwezi jua wameona nini, maana wameniambia wanahitaji kufanya mabadiliko na mimi nimelipokea vizuri hilo suala, nimemalizana nao vizuri na niwatakie kila la kheri, waendelee kupambana zaidi wafikie malengo waliyojiwekea.
“Kikubwa timu inapaswa iendelee kupambana hata kama akiondoka nani kwenye timu, ningependa wachezaji waendelee kujitoa zaidi ya hata nilipokuwa mimi naiongoza timu ili malengo yafikiwe,” alisema Katwila aliyeanza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2020.
Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ameiongoza Ihefu kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na kuifunga Yanga mabao 2-1 huku ikifungwa na Geita Gold bao 1-0, ikichezea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mashujaa kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 mbele ya KMC.
Ihefu inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi sita, tofauti ya pointi tisa dhidi ya kinara wa msimamo wa ligi Simba SC yenye pointi 15 pia ikiwa ni tofauti ya pointi nne dhidi ya Coastal Union inayoburuza mkia kwa pointi mbili pekee.