Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Ally Mayay (pichani) amesema serikali imejiandaa vya kutosha kuhakikisha tukio la ufunguzi la African Football League (AFL) kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam linaweka rekodi na historia kubwa duniani.
Mayay amezungumza hayo leo Alhamisi zikiwa zimesalia takribani ziku saba kabla ya ufunguzi rasmi wa ligi hiyo itakayoanza kwa Simba SC kuumana na Al Ahly ya Misri Oktoba 20, mwaka huu.
Uzinduzi wa ligi hiyo mpya kabisa Afrika inayoshusisha timu nane utahudhuriwa na ugeni wa Rais wa Fifa, Gianni Infantino na viongozi wengine wakubwa wa soka Afrika, hivyo Mayay amesisitiza lazima liwe tukio la rekodi.
“Sisi tulishajipanga kwa muda mrefu, kwenye mashindano ya kimataifa achilia mbali mashindano makubwa kama Afcon lakini hata mashindano haya ya AFL ambayo yanaweka historia ya kuzinduliwa nchini lazima kuna kitu kinapangwa kwa ajili ya kuthibitisha utayari wa serikali katika matukio makubwa kama haya.
“Kinachoendelea pale Kwa Mkapa ni maandalizi ya kuhakikisha tukio hili litaweka rekodi na watu wataendelea kukumbuka kwamba Tanzania siku ya uzinduzi kilifanyika hiki na hiki sababu Dunia itakuwa makini siku hiyo kuifuatilia Tanzania,” alisema Mayay.
Alisema mpaka sasa media (vyombo vya habari) zote kubwa duniani zinafuatilia tukio hilo ambalo anaamini litaitangaza nchi na kwa uzinduzi huo wa kihistoria utakaofanyika Dar es Salaam, Tanzania.
Mbali ya Simba na Al Ahly ambao watacheza mechi ya marudiano Oktoba 23, mwaka huu jijini Cairo, mechi za robo fainali nyingine zitawakutanisha TP Mazembe dhidi ya Esperance, Enyimba dhidi ya Wydad CA na Petro du Luanda itaumana na Mamelodi Sundowns.