New York, Marekani
Nahodha wa Inter Miami FC ya Marekani. Lionel Messi hatojiunga na klabu yoyote kwa mkopo wakati msimu wa Ligi Kuu ya Soka Marekani (MLS) utakapofikia mwisho.
Kauli hiyo iliyotolewa na mchambuzi na mdau maarufu wa soka, Guillem Balague inakuwa imefuta habari zilizokuwapo kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 angejiunga na Barcelona na baadaye kwenda Saudi Arabia.
Messi ambaye kwa sasa ni majeruhi mechi yake ya mwisho na Inter Miami alicheza kwa dakika 72 kabla ya kutolewa na Jumamosi iliyopita timu yake ililala kwa bao 1-0 mbele ya FC Cincinnati.
Msimu wa MSL unafikia ukomo Oktoba 21 huku habari zikiwapo kwamba baada ya msimu huo, Messi angeuzwa kwa mkopo na klabu ambayo imekuwa ikitajwa zaidi ni Barcelona aliyowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa MLS, Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina atakuwa na kibarua kwenye timu yake ya taifa itakayokuwa na mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Uruguay Novemba 17 na Brazil Novemba 22 na baada ya.hapo atakuwa na mapumziko zaidi ya mwezi mmoja.
“Messi atakuwa na likizo ya kama kama wanasoka wengine kwa hivyo msahau kuhusu kwenda Saudi Arabia au kwingineko,” alisema Balague.